January 11, 2011

Ngeleja ‘aonja sauti’ za wafanyakazi TANESCO

  • ·      Aahidi kushughulikia kero za TANESCO
  • ·      Hatma ya ‘staff rate’ yabaki mikononi mwa TANESCO
  • ·      Mikataba mibovu yawakera wafanyakazi
  • ·      Asisitiza ubunifu ndani ya Shirika

Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.William Mganga Ngeleja mwishoni mwa wiki alitembelea Ofisi za TANESCO Makao Makuu zilizopo Ubungo jijini Dar es Salaam kwa nia ya kuzungumza na viongozi na wafanyakazi wa Shirika hilo.

Katika msafara huo, Mhe.Ngeleja aliandamana na Naibu Waziri wake Mhe. Adam Malima na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali kutoka wizara hiyo.

Waziri Ngeleja katika hotuba yake kwa viongozi na wafanyakazi wa TANESCO alisema kipaumbele cha wizara yake na TANESCO, ni kuhakikisha kuwa wanarudisha imani kwa wateja iliyopotea kuhusu utoaji wa huduma ya nishati nchini.

Ngeleja alizitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili wizara ambazo pia baadhi zilitajwa kwenye hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi William Mhando kama, kushindwa kuzalisha umeme wa kutosha unaokidhi mahitaji ya wateja kwa bei nafuu, kiwango kidogo cha wananachi wanaopata huduma ya umeme kwa sasa (14.2%) na uchakavu wa miundombinu.

Changamoto nyingine ni ucheleweshwaji wa utekelezeji miradi kulingana na Mpango Mkakati wa Shirika (2010), ufinyu wa bajeti na utoaji wa elimu kwa umma kuelewa mipango iliyopo kuhusu ili kuondokana na tatizo la mgao wa umeme.

Pamoja na miradi iliyopo, waziri Ngeleja alisisitiza azma ya serikali kuanza mipango ya kutumia madini ya uranium kuzalisha umeme mwaka 2012, mipango ya kuboresha miundombinu, kujenga kituo cha megawati 230 Somanga Fungu kinachotumia gesi asilia na Kituo kinachozalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe cha megawati 400 Liganga, Mchuchuma.
Mipango mingine ni Rumakali megawati 222 na Stiglers Gorge ambayo ameahidi itakamilika ndani ya miaka mitano 2010-2015 ya uongozi wake.

Katika hotuba yake pia alitoa maelekezo kwa Bodi ya wakurugenzi ya TANESCO kusimamia na kuangalia kama mfumo wa kiutendaji wa Shirika unakidhi mikakati ya Mpango wa biashara (2010) uliopo, kuimarisha kitengo cha sheria ilikiweze kutoa ushauri sahihi kwenye masuala ya mikataba na kuimarisha mawasilino baina ya Shirika na wizara.

Aidha aliwataka wafanyakazi wa TANESCO kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi yao wenyewe kama vile kuandika michanganuo ya kutaka kuanzisha kituo cha kuzalisha umeme kwa maji na serikali itasaidia.

Alishauri TANESCO kutenga bajeti ya kutosha kuhusu elimu kwa umma. TANESCO itumie vyombo vya habari kueleza wananchi na kuwaelimisha kuhusu shughuli inazofanya.
Akijibu baadhi ya maswali na hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Majadiliano, Waziri Ngeleja aliahidi kushughulikia kero zote zinazowakwaza wafanyakazi wa TANESCO ikiwemo mali za Shirika ambazo zinatumiwa isivyo halali.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi William Mhando alielezea jitihada zinazofanywa na TANESCO katika kuikwamua nchi na tatizo la umeme.

Alielezea mafanikio ambayo Shirika limeyafikia na jitihada ambazo zinafanywa ilikuona kuwa TANESCO inatoa huduma bora kwa wateja wake.

Baadhi ya changamoto ambazo Mhandisi Mhando alizitaja ni kutokomeza vishoka, upatikanaji wa vifaa vya kuwaunganisha wateja, ukusanyaji wa madeni, uwezo mdogo wa kuzalisha umeme, upotevu wa umeme, gharama za uzalishaji umeme, sheria mpya ya manunuzi ya mwaka 2004 na kuchakaa kwa mashine na miundombinu.

Mhandisi Mhando alitaja mipango ya muda mfupi iliyopo kwenye Idara ya Uzalishaji umeme kama, kujenga kituo cha kuzalisha umeme cha megawati 100 Dar es Salaam, megawati 60 Mwanza, megawati 300 Mnazi Bay (gesi asilia) , Kiwira megawati 200 (Makaa ya mawe), Kinyerezi megawati 240 na Singida megawati 100 (upepo).

Aidha alisema, Idara ya Usafirishaji umeme ina mipango ya kujenga njia kuu za kusafirisha umeme kutoka Iringa-Shinyanga ya msongo wa kilovolti 400, Shinyanga – Geita 220kV, Makambako - Songea 132kV, Mnazi Bay – Singida 400 DC kV, mipango ambayo itaambatana na uboreshaji wa kituo cha SCADA.

Kwenye usambazaji umeme, Mhandisi Mhando alitaja miradi ya TEDAP, MCC unaotekelezwa kwenye mikoa sita ya nchini, ADB na kuboresha mifumo ya usambazaji umeme katikati ya jiji la Dar es Salaam inayosimamiwa na wa Finland kama miradi ambayo itaboresha sana huduma ya usambazaji umeme nchini.

Miradi mingine ni ile ya ufungaji wa AMR, kuunganisha wateja 100,000, kuanzishwa kituo cha miito, kufunga mita za LUKU na utoaji wa elimu kwa wafanyakazi.

Akihitimisha hotuba yake Mhandisi Mhando alisema, Shirika limejipanga kukabiliana na changamoto zilizopo na kuiomba wizara iendelee kutoa ushauri kwa TANESCO ili iweze kutoa huduma bora zaidi.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Majadilinao Bw. Abdul Mkama akitoa hotuba yake kwa niaba ya wafanyakazi alimuomba waziri kuishauri serikali itoe misaada kwa TANESCO ya sasa yenye uongozi wa wazawa kama ilivyokuwa inatoa wakati wa Net Group Solutions.

Pia aliiomba serikali kulipa medeni yake na taasisi zake ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini na deni la Zanzibar.

Aliiomba serikali kuona jinsi ya kuondoa kodi kwenye mafuta na vifaa vya umeme vinavyoagizwa kutoka nje ilikumpunguzia gharama mteja mzigo na serikali kuepuka mikataba mibovu ambayo inalipa hasara kubwa shirika na hivyo kuwakatisha tamaa wafanyakazi.

Kuhusu suala la kuondolewa kwa ‘staff rate’ ambalo waziri katika hotuba yake alisema limeamuliwa na chombo chenye mamlaka kisheria, Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Majadiliano alisema suala hilo lipo ndani ya uwezo wa TANESCO na uongozi kwani limewekwa kisheria na lipo kwenye mkataba wa hiari. Hivyo linazungumzika wala wafanyakazi wasiwe na wasiwasi.
Kikao hicho ni cha kwanza cha aina yake tangu Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Willam Ngeleja kuchaguliwa tena na rais kushika wadhifa huo Desemba 2010.


Mh. William Ngeleja(wa pili kushoto) akipata maelezo kuhusu namna ya kusoma mita kupitia teknolojia ya AMR (Automatic Meter Reading). Kushoto ni Naibu Waziri Wizara ya Nishati na Madini, Mh. Adam Malima

Mh. William Ngeleja(wa pili kulia) akipata maelezo kuhusu uendeshaji wa  kituo cha miito ya simu TANESCO Makao Makuu.Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi William Mhando.

Mh. William Ngeleja(kushoto) akiangalia mfumo maalum wa computer unaotumika kuhifadhi kumbukumbu (computer server).

Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi William Mhando (kushoto) akihutubia wafanyakazi.Kutoka kulia ni Waziri wa Nishati na Madini Mhe. William Ngeleja, na Naibu wake Mhe. Adam Malima

Waziri wa Nishari na Madini, Mhe. William Ngeleja akiwasalimu wafanyakazi wa TANESCO  mara baada ya mkutano huo kumalizika.

Mmoja wa wafanyakazi walimuuliza maswali Mhe. Ngeleja akisoma kifungu cha Biblia ili kutilia mkazo katika maswali aliyouliza.

Waziri wa Nishati na Madini Mhe. William Ngeleja akisisitiza jambo wakati akihutubia wafanyakazi wa TANESCO.

Mwenyekiti wa kamati ya majadiliano TUICO Bw. Abdul Mkama akisisitiza jambo wakati akitoa hotuba yake kwa niaba ya wafanyakazi kwa Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. William Ngeleja.

Kutoka kushoto, Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.William Ngeleja, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi William Mhando pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sao Hill wakibadilishana mawazo mara baada ya mkutano huo.

No comments:

Post a Comment