August 30, 2011

MATATIZO YA MFUMO WA KUUZA UMEME KWENYE VITUO VYA LUKU


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linasikitika kuwafahamisha wateja wake wote wanaotumia mita za LUKU kuwa tangu jana mchana (29/08/2011) kumejitokeza matatizo ya kiufundi kwenye vituo vya uuzaji umeme.  Matatizo haya yamesababisha mfumo mzima wa kuuzia LUKU kutofanya kazi.

Mafundi wa TANESCO walikuwa wanashughulikia tatizo hilo ili uuzaji umeme wa LUKU urejeshwe katika hali yake ya kawaida haraka iwezekanavyo..

Uongozi wa Shirika unaomba radhi kwa usumbufu wowote uliojitokeza.

 


IMETOLEWA NA OFISI YA UHUSIANO


TANESCO MAKAO MAKUU

August 12, 2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kuuarifu umma kuwa mitambo mipya ya kuzalisha umeme ya Megawati 100 iliyoahidiwa bungeni na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa William Ngeleja, imewasili nchini leo na kazi ya kuifunga inaanza mara moja.

Mitambo hiyo iliyokodiwa kutoka Kampuni ya Aggreko ya Mombasa (Kenya), itafungwa katika maeneo ya Ubungo na Tegeta jijini Dar es Salaam ambapo kila kituo kitazalisha Megawati 50.

Umeme wa mitambo hiyo utaingia kwenye gridi ya Taifa mapema Septemba 2011.

Mitambo hiyo itakayotumia mafuta itapunguza  kwa kiasi kikubwa tatizo la mgawo wa umeme nchini kwa kuzingatia ukweli kuwa mitambo ya Jacobsen Electro Supply kutoka Sweden itakayozalisha Megawati 100 nayo imeshaanza kufungwa Ubungo.

Awali TANESCO ilikuwa ikikabiliwa na upungufu wa Megawati 260. Hivyo kuwasili kwa mitambo ya Aggreko, kuwashwa mitambo ya IPTL inayozalisha Megawati 100, kutumika kwa Mitambo ya Symbion ya Megawati 112  na kuendelea kufungwa mitambo ya Jacobsen kunaipa TANESCO nafasi kubwa ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme mara baada ya kazi ya ufungaji wa mitambo hiyo itakapokamilika.

TANESCO inapenda kuwahakikishia Watanzania kwamba inafanya kila jitihada kuhakikisha kuwa Mikoa yote iliyounganishwa katika gridi ya Taifa inapata umeme wa kutosha, sambamba na kupanua huduma ya usambazaji umeme kwa wateja wapya.


Imetolewa na:             OFISI YA UHUSIANO,      
                                    TANESCO  -  MAKAO MAKUU.