February 21, 2018

"SERIKALI IMEKIONGEZEA UWEZO KITUO CHA KUFUA UMEME CHA MTWARA" NAIBU WAZIRI NISHATI




Naibu Waziri Nishati Mhe. Subira Mgalu (MB), amekagua mashine mbili zenye uwezo wa kufua jumla ya Megawati nne (4) zitakazofungwa katika kituo cha kufua umeme kwa ktumia  gesi asilia cha "Mtwara Gas Plant".

Katika ziara hiyo, Mhe. Mgalu aliambatana na Viongozi wa Wizara, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TANESCO Dkt. Alexander L. Kyaruzi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mhandisi Khalid James na Uongozi wa TANESCO Kanda ya Dar es Salaam na Pwani.

Alisema, Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) inaendelea kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa umeme Mikoa ya Mtwara na Lindi na hatua mojawapo zinazochukuliwa ni kukiongezea uwezo kituo hicho.

Aliongeza, kituo cha Mtwara kina miaka kumi (10) tangu kujengwa kwake na kina jumla ya mashine tisa (9) zenye uwezo wa kufua Megawati 18, na kwa juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati  zinaongezwa mashine mbili zenye uwezo wa kufua Megawati nne (4) hivyo kufikia Jumla ya Megawati ishirini na mbili (22).

"Kutokana na kukua kwa mahitaji ya umeme kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi, Serikali iliona ipo haja ya kuongeza mashine nyingine mbili zenye uwezo wa kufua Megawati nne ili ziungane na zilizopo na hivyo kufikisha Megawati ishirini na mbili ambazo zitakuwa na uwezo wa kutosheleza mahitaji katika Mikoa ya Mtwara na Lindi". Alisema Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mahitaji ya juu ya umeme kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi ni zaidi ya Megawati 16, hivyo ujio wa mashine hizi unatarajiwa kuimarisha zaidi hali ya upatikanaji wa umeme katika Mikoa hiyo.









No comments:

Post a Comment