September 15, 2018

TANESCO KUOKOA ZAIDI YA SH. MILIONI 450 KILA MWEZI BAADA YA MITAMBO YA UMEME WA DIZELI SONGEA KUZIMWA

 Moja ya mitambo ya kufua umeme wa mafuta ya dizeli uliokuwa kwenye kituo cha Songea ikiwa imezimwa.

 NA K-VIS BLOG, SONGEA

KUTOKANA na kuzimwa kwa mitambo ya dizeli iliyokuwa ikitumika kufua umeme kwa matumizi ya mji wa Songea na vitongoji vyake Septemba 13, 2018 baada ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, Shirika la umeme Tanzania TANESCO sasa litaokoa kiasi cha zaidi ya shilingi Milioni 450,108,508 zilizokuwa zikitumika kununua dizeli kila mwezi.


Septemba 13, 2018 TANESCO iliwasha rasmi kituo kipya na cha kisasa cha kupoza na kusambaza umeme cha Madaba, ambacho kimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa na hivyo kuondoa matumizi ya umeme wa mafuta kwenye Halmashauri ya Manispaa ya mji wa Songea na vitongoji vyake.


Kuwashwa kwa mtambo huo ni baada ya kukamilika kwa Mradi wa umeme wa Makambako-Songea ambao ulihusisha ujenzi wa vituo vya kupoza na kusambaza umeme vya Makambako na Songea sambamba na upanuzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Makambako, lakini pia Ujenzi wa njia kuu ya usafirishaji Umeme wa kilovoti 220 yenye urefu wa kilometa 245 kutoka Makambako hadi Songea kupitia Madaba. Usambazaji Umeme wa msongo wa 33kV zenye urefu wa kilomita 900 na kuunganisha wateja 22,700 katika Wilaya za Njombe , Ludewa na mji wa Makambako katika Mkoa wa Njombe, Songea Vijijini, Songea Mjini, Namtumbo na Mbinga katika Mkoa wa Ruvuma.

Tayari wakazi wa mji wa Songea wamepokea taarifa za mji wao kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa na hivyo kuondoa ile adha ya kukatika umeme iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu. 

Songea kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kuna maanisha mji huo sasa umeanza kupata umeme ulio bora na wa uhakika na hivyo wananchi sasa wanapaswa kuchangamkia fursa ya uwepo wa nishati hiyo kwa kufungua viwanda vidogo na miradi mbalimbali ya kiuchumi inayotegemea nishati ya umeme.
 Kituo cha Umeme TANESCO Songea ambacho kilikuwa kikitumia mashine zinazoendeshwa kwa mafuta ya dizeli. Kituo hicho sasa kimezimwa.
 Tenki la kuhifadhia mafuta ya dizeli, ambalo sasa litabaki kama kumbukumbu, baada ya matumizi yake kukoma rasmi Septemba 13, 2018.

No comments:

Post a Comment