Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizindua Mradi 
wa Ujazilizi Umeme Vijijini fungu la pili A katika Kijiji cha Bukene, 
Wilayani Nzega Mkoani Tabora, amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya 
Shilingi bilioni 190.7 kufikisha Umeme kitongoji kwa kitongoji katika 
vitongoji 1,103 vya Mikoa 9.
Waziri Kalemani aliitaji Mikoa hiyo ambayo vitongoji vyake vitanufaika 
moja kwa moja na mradi huo kwa sasa kuwa ni, Mikoa ya Dodoma, Tabora, 
Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Singida, Pwani, Mbeya pamoja na Tanga.
“Uzinduzi huu wa Mradi wa Ujazilizi Fungu la pili A ni muendelezo wa 
usambazaji Umeme kwa Wananchi wote. Kazi hii bado inaendelea, ndani ya 
miaka miwili toka sasa, tutakuwa tumevifikia Vijijini vyote takriban 
12,304 na Vitongoji vyake vyote 64,839 Nchini” Alisema Dkt. Kalemani
Waziri Kalemani aliendelea kwa kuwataka Watanzania ambao hawajafikiwa na
 huduma ya Umeme kuwa watulivu kwani lengo na mipango ya Serikali ni 
kuwafikishia Wananchi wote umeme ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo 
ndani ya kipindi cha miaka miwili toka sasa. 
“Tumepeleka umeme kijiji kwa Kijiji na sasa tunakaribia kumaliza vijiji 
vyote Nchini, sasa tunakwenda kitongoji kwa kitongoji, kaya kwa kaya 
mpaka tutakapowafikia Wananchi wote” Alieleza Dkt. Kalemani
Kwa upande wa Wananchi wa Bukene, waliohudhuria katika uzinduzi huo 
walionesha kufurahishwa na kufarijika sana na mradi huo wa ujazilizi 
kuanzia na kuzinduliwa kitaifa katika kijiji na vitongoji vyao vya 
kijiji cha Bukene Migombani. 
Naye Mwandu Igusule, mkazi wa eneo la Bukene, alisema kuwa wanatarajia 
kuutumia umeme huo kwa maendeleo yao ya kijamii pamoja na kujikwamua 
kiuchumi kwa kuanzisha miradi na shughuli mbalimbali zinazotegemea 
Nishati ya Umeme.









