September 25, 2020

"UMEME SASA NI KITONGOJI KWA KITONGOJI" DKT. KALEMANI

 


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizindua Mradi wa Ujazilizi Umeme Vijijini fungu la pili A katika Kijiji cha Bukene, Wilayani Nzega Mkoani Tabora, amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya Shilingi bilioni 190.7 kufikisha Umeme kitongoji kwa kitongoji katika vitongoji 1,103 vya Mikoa 9.

Waziri Kalemani aliitaji Mikoa hiyo ambayo vitongoji vyake vitanufaika moja kwa moja na mradi huo kwa sasa kuwa ni, Mikoa ya Dodoma, Tabora, Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Singida, Pwani, Mbeya pamoja na Tanga.

“Uzinduzi huu wa Mradi wa Ujazilizi Fungu la pili A ni muendelezo wa usambazaji Umeme kwa Wananchi wote. Kazi hii bado inaendelea, ndani ya miaka miwili toka sasa, tutakuwa tumevifikia Vijijini vyote takriban 12,304 na Vitongoji vyake vyote 64,839 Nchini” Alisema Dkt. Kalemani

Waziri Kalemani aliendelea kwa kuwataka Watanzania ambao hawajafikiwa na huduma ya Umeme kuwa watulivu kwani lengo na mipango ya Serikali ni kuwafikishia Wananchi wote umeme ambao bado hawajafikiwa na huduma hiyo ndani ya kipindi cha miaka miwili toka sasa.

“Tumepeleka umeme kijiji kwa Kijiji na sasa tunakaribia kumaliza vijiji vyote Nchini, sasa tunakwenda kitongoji kwa kitongoji, kaya kwa kaya mpaka tutakapowafikia Wananchi wote” Alieleza Dkt. Kalemani

Kwa upande wa Wananchi wa Bukene, waliohudhuria katika uzinduzi huo walionesha kufurahishwa na kufarijika sana na mradi huo wa ujazilizi kuanzia na kuzinduliwa kitaifa katika kijiji na vitongoji vyao vya kijiji cha Bukene Migombani.

Naye Mwandu Igusule, mkazi wa eneo la Bukene, alisema kuwa wanatarajia kuutumia umeme huo kwa maendeleo yao ya kijamii pamoja na kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi na shughuli mbalimbali zinazotegemea Nishati ya Umeme.

 






No comments:

Post a Comment