November 11, 2020

JNHPP - Zoezi la kuchepusha Maji kuanza

Kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa handaki la kuchepusha maji katika mradi wa Julius Nyerere, kazi inayofuatia ni uchepushaji wa maji ili kuanza ujenzi wa tuta kuu.

Handaki hilo lina urefu wa mita 703 na upana wa mita 17 huku kimo chake kikiwa mita 12.

Akiongea kuhusu kufikiwa kwa hatua hiyo muhimu, Mhandisi Said Kimbanga ambaye ni Meneja Ujenzi, amesema zoezi linalofanyika kwa sasa ni utoaji wa udongo kwenye njia ya kuingilia maji, kufikia kwenye level ya 68.5 juu ya usawa wa bahari ili maji yaweze kupita.

"Hapa tulipo maji yanapita kuelekea baharini, hatuwezi kujenga tuta kuu hadi tutakapo yachepusha maji kupita kwenye handaki na eneo hilo kubaki kavu" alisema Mhandisi Kimbanga.

Aliongeza handaki hilo limekamilika kwa asilimia 100, zoezi linaloendelea ni uondoaji wa vifaa ndani ya handaki na kukata udongo uliopo mbele ya lango la kuingilia maji ili kuruhusu maji kuingia ndani ya handaki.

Aidha, zoezi lingine litakalofanyika ni ujazaji wa udongo kwenye mto kujenga tuta (cofferdam) ili kufunga mto na kuruhusu maji kupita kwenye handaki mchepusho.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano TANESCO, Johary Kachwamba amesema kukamilika kwa mradi wa Julius Nyerere Tanzania itakuwa na umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.

"Umeme unaozalishwa kwa maji ni umeme wa bei nafuu, kutokana na umeme wa maji kuzalishwa kwa gharama kidogo hivyo tutarajie bei ya umeme kwa Wateja kushuka" amesema Kachwamba.

Aliongeza, kutokana na umeme wa maji kuwa wa gharama nafuu ambapo unit moja inazalishwa kwa shilingi 36 TANESCO itaweza kujiendesha kwa faida zaidi.

"Tanzania inaelekea sehemu ya kihistoria, kwa kuwa na maendeleo endelevu, tutaokoa mazingira kwani wananchi wataweza kumudu gharama za umeme hivyo kuondoa matumizi ya kuni na mkaa" alisisitiza Kachwamba.
 


 
 


 

No comments:

Post a Comment