November 29, 2010

MGAO WA DHARURA KWA MIKOA ILIYO KATIKA GRIDI

Kufuatia kutokea kwa hitilafu za kiufundi kwa baadhi ya mashine katika mitambo ya Songas, Ubungo na kuisha kwa mafuta katika mtambo wa IPTL shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), limelazimika kufanya mgawo wa umeme kwa mikoa iliyoungwa katika gridi ya taifa.

Aidha, mitambo ya New Pangani na Kihansi nayo imepunguza uzalishaji kutokana na kupungua kwa kina cha maji.

Kutokana na hali hiyo Shirika limelazimika kufanya mgawo wa dharura ambao huenda ukaisha wakati wowote kuanzia wiki ijayo kutokana na jitihada zinazofanywa kunusuru hali hiyo kuendelea.

Miongoni mwa jitihada zinazofanywa ni kutengeneza kwa mashine hizo haraka na kukamilisha taratibu za kununua mafuta kwa ajili ya kuendesha mtambo wa IPTL. Hata hivyo, taratibu za kununua mafuta zinatarajiwa kukamilika wiki hii ili Jumatatu mafuta yaweze kupatikana haraka na kupelekwa IPTL kwa ajili ya kuendesha mtambo huo.

Ratiba ya mgawo inatarajiwa kutolewa baadaye na tunawasihi wateja wetu na wananchi kwa ujumla kuwa na subira wakati jitihada zinafanywa kukabiliana na mgawo huo wa dharura.

Badra Masoud,
MENEJA MAWASILIANO.

No comments:

Post a Comment