March 1, 2018

Mhe. Mgalu awasihi Wananchi Mkoani Shinyanga kuupokea mradi wa Umeme Vijijini


Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu,  amefanya ziara ya kikazi katika Vijiji Vitakavyopitiwa na Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) na vile vilivyopendekezwa katika Mradi kabambe wa kuongeza wigo (REAII Densification) vilivyopo Mkoani Shinyanga.

Katika Ziara hiyo, Mhe. Mgalu  aliwasihi Wananchi kuupokea mradi huo na kuongeza kuwa Serikali itahakikisha Vijiji vyote vilivyobakia wilayani humo vitapata umeme kufikia 2020.

Aidha, Naibu Waziri alitumia ziara hiyo kukitambulisha kifaa cha Umeme Tayari  (UMETA) na kuwasihi Wananchi kujitokeza kwa wingi pindi mradi wa "Densification" utakapoanza  na kuitaka TANESCO kuhakikisha inashirikiana kwa karibu na Viongozi wa Serikali katika ngazi zote ili kuhakikisha miradi kwenye Vijiji vyote  unatekelezwa kwa weledi huku vipaumbele ikiwa ni Taasisi za Serikali na zile za Kidini.

 Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi FedGrace Shuma alimhakikishia Naibu Waziri kuwa, atahakikisha miradi katika Vijiji vyote unakamilika kwa ufanisi kama ambavyo Serikali imeagiza, kwa kuzingatia huduma iliyoboreshwa.
 
Katika ziara hiyo Naibu Waziri aliambatana na Wakuu wa Wilaya za Kahama na Shinyanga, REA, TANESCO (Mkoa na Kanda) Viongozi wengine wa Serikali Mkoa na Wilaya pamoja na wadau kutoka Taasisi zingine Wilayani Kahama na Shinyanga.





No comments:

Post a Comment