November 18, 2019

Dkt. Medard Kalemani Ahamasisha Wawekezaji wa Migodi



Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani Ahamasisha Wawekezaji wa Migodi, Hoteli na Viwanda kuunganisha umeme wa bei nafuu Wa TANESCO Mkoani Mara ili kuongeza ufanisi pamoja na kuboresha zaidi biashara zao ambapo amesema kuwa, TANESCO tayari inapeleka umeme mwingi wa takriban Megawati 82 Mkoani humo lakini matumizi ya Mkoa mzima kwa sasa ni takriban Megawati 33 ambazo ni chache mno ukilinganisha na shughuli za kiuchumi zilizopo mkoani humo.

Waziri Kalemani aliyasema hayo alipotembelea Mkoa huo kwa ziara ya kikazi ya kukagua na kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Umeme Mkoani humo hususan Miradi ya umeme Vijijini pamoja na Mijini.

‘’Mkoa wa Mara, una fursa mbalimbali za kimaendeleo ikiwemo Viwanda, Mahoteli na raslimali kubwa ya madini na migodi mingi ambayo bado haijaunganishwa na umeme wa gharama nafuu wa TANESCO na wanatumia vyanzo ghali vya Umeme wa mafuta kuendesha biashara zao’’, Alisema Dkt. Kalemani

Aidha Dkt. Kalemani aliagiza, TANESCO Mkoa wa Mara na Mikoa mingine ambayo bado matumizi ya umeme yako chini, ukilinganisha na umeme unaopatikana maeneo hayo kuhakikisha kuwa wanaanzisha kampeni kabambe ya mlango kwa mlango kutembelea Wawekezaji na Wafanyabiashara wote katika maeneo yao ambao bado hawajaunganisha umeme wa TANESCO ili kuwaelimisha na kuwahamasisha kuunganisha umeme wa TANESCO kwani hivi umeme wa TANESCO ndio chanzo nafuu kabisa cha Nishati, ambayo imesambaa maeneo mengi Nchini na ndio Nishati ya uhakika na unaotabirika kwa sasa.

Aliongeza kuwa kwa kutumia Umeme Nafuu wa TANESCO, itawezesha gharama za uzalishaji mali na uendeshaji kupungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kuchochea zaidi ukuwaji wa shughuli hizo kwa ujumla ikiwemo viwanda, Migodi, Mahoteli na Shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii ambazo pia zitachochea ukuwaji wa Uchumi wa Taifa zima kwa ujumla.




No comments:

Post a Comment