WAZIRI
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani leo Novemba 15, 2019 amezindua Bodi ya
Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) aliyoiteua juzi
Novemba 13, 2019.
Dkt.
Kalemani akiambatana na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu, ameizundia
Bodi hiyo yenye wajumbe 9 juzi jijini Dodoma na kuipa maagizo
yapatayo 16.
Bodi
hiyo itaongozwa na Dkt. Alexander Kyaruzi ambaye aliteuliwa Novemba
9, 2019 na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kipindi kingine cha pili kuongoza Bodi
hiyo.
Akizindua Bodi hiyo itakayodumu kwa miaka mitatu, Dkt. Kalemani alimemkabidhi
Mwenyekiti Dkt. Kyaruzi kitendea kazi ambacho ni Sheria ya Umeme ya
Mwaka 2008 aliyosema ndiyo itakayowaongoza katika majukumu yao.
Aidha, aliwapa
maelekezo ya kuwa umeme ndio injini ya uchumi wa viwanda hivyo ni
lazima waisimamie Tanesco kuhakikisha umeme unapatikana katika shughuli
zote za kiuchumi nchini. Alitaka uwepo umeme wa kutosha na unaotabirika
ili kufanikisha azma hiyo ya Serikali.
Aliwataka
wakasimamie miradi hiyo iliyoanza kutekelezwa na itakayotelezwa na
Tanesco, na katika hilo, wahakikishe Mradi wa Kufua Umeme wa Maporomoko
ya Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) katika mto Rufiji wa megawati 2,115,
unakamilishwa kwa wakati ifikapo Juni 14, 2022, kama ilivyoelezwa katika
mkataba.
Aliitaja
miradi mingine kama wa Ruhuji megawati 358, Rumakari megawati 222 na
Malagarasi na mengine, inasimamiwa na kukamilika kwa wakati.
Aliwataka
kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 njia zote za kusafirishia umeme
zinaunganishwa na Gridi ya Taifa katika kona zote za Tanzania, kwa
kuhakikisha asilimia 85 ya Watanzania wawe wameanza kutumia umeme
wakiwamo wale wanaoishi vijijini.
Dkt.
Kalemani pia aliitaka bodi kuhakikisha wanarekebisha, wanaboresha na
kuimarisha miundombinu ya usafirisha umeme, kuisimamia TANESCO na Wakala
wa Umeme Vijijini (REA) katika miradi ya umeme vijijini kwa kuwabana
makandarasi kukamilisha miradi kwa wakati.
“Tusingependa
kuongeza hata dakika moja kwa mkandarasi katika mradi wowote ule,
tunataka wakabidhi miradi kwa wakati,” alisema Dkt. Kalemani.
Aidha,
aliitaka bodi kuhakikisha viwanda vinapata umeme wa uhakika kwa kutumia
transfoma kubwa zenye uwezo wa kuchukua umeme mwingi, na pia kusisitiza
mita, transfoma, na nyaya haziuzwi kwa mwananchi yeyote na atakayekiuka
agizo hilo achukuliwe hatua.
Alisisitiza
kuwa kwa vijijini, mwananchi aunganishiwe umeme kwa Sh 27,000 tu, na
atakayekiuka hilo, naye achukuliwe hatua na bodi kwa yule aliye kwenye
mamlaka yao.
Kuhusu
mapato ya shirika, alitaka wasimamie ukusanyaji huo wa mapato, na
kuagiza kuwa kwa yeyote ambaye anadaiwa Ankara na Tanesco akatiwe huduma
mara moja na hasa kama madeni hayo ni sahihi na halali.
Aliagiza
pia kuyaaangalia maeneo yenye tija kama viwanda, mitambo ya kusukuma
maji, zahanati na mengine na kukusanya mapato, huku akiisifu Tanesco kwa
kuongeza mapato kutoka Sh bilioni 9 hadi kufikia Sh bilioni 46 na
kutaka waongeze bidii ifike Sh bilioni 60.
Aidha,
aliwataka kuongeza vyanzo vya mapato, kuondoa kero ya watu wanaosubiri
kuunganishiwa umeme kwani nguzo na nyaya zipo za kutosha, kudhibiti
vishoka wachache waliopo, kuhakikisha katikakatika ndogo ya umeme
iliyopo inakuwa historia na kuwajengea uwezo wazalishaji wadogo wa umeme
nchini.
Mbali
ya kuwataka kuwa wabunifu na wenye uthubutu kwa kufanya kazi kwa
kuzingatia kasi, wepesi na nidhamu, aliwaagiza kuwa sheria za manunuzi
zisiwe kificho cha kuchelewesha kazi.
Kuhusu
Jiji la Dodoma, aliagiza liangaliwe kwa ukaribu na kila eneo lipate
huduma ya umeme, na hilo anataka kuliona limefanyika ndani ya miezi
sita.
Katika
utekelezaji wa hayo yote, Dkt. Kalemani ameagiza Bodi itoe taarifa
kwa wizara kila baada ya miezi mitatu kuelezea utendaji wao wa kazi.
Naibu
Waziri Mgalu kwa upande wake, aliwatakia kila la heri wajumbe wa bodi
hiyo, na kueleza kuwa wizara inawategemea sana katika kusukuma mbele
majukumu hasa ya kulisimamia shirika hilo la TANESCO.
No comments:
Post a Comment