Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeelezea sababu za uwepo wa upungufu wa umeme kuwa unasababishwa na ukame pamoja na matengenezo kinga na marekebisho makubwa kwenye vituo na mitambo, na kusababisha upungufu wa jumla ya megawati 300 hadi 350 za umeme kwa siku za hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Maharage Chande alisema upungufu wa umeme unasababishwa na ukame pamoja na matengenezo ya mitambo.
“Upungufu huu unasababishwa na mambo makubwa mawili, ukame mkubwa ambao nchi yetu inapitia na matengenezo kinga na marekebisho makubwa ya mitambo ambayo ni lazima yafanyike” alifafanua Bw. Chande.
Aidha, Bw. Chande aliviainisha vituo vya kufua umeme vilivyoathiriwa na ukame ambavyo ni Kihansi kinachozalisha megawati 17 badala ya megawati 180 kwa hiyo megawati 163 hazizalishwi; Pangani kinachozalisha megawati 10 badala ya megawati 68 kwa hiyo megawati 58 hazizalishwi.
Vituo vingine ni Mtera kinachozalisha megawati 75 badala ya megawati 80 kwa hiyo megawati 5 hazizalishwi na Nyumba ya Mungu kinachozalishaji megawati 3 badala ya megawati 8 za umeme, kwa hiyo megawati 5 hazizalishwi.
Vilevile, Bw. Chande alivitaja vituo vilivyo katika matengenezo kinga kuwa ni Kidatu kinachozalisha megawati 150 badala ya megawati 200, kwa hiyo megawati 50 hazizalishwi; Ubungo III kinachozalisha megawati 37 badala ya megawati 112, kwa hiyo megawati 75 hazizalishwi.
Kituo kingine ni Kinyerezi II kinachozalisha megawati 205 badala ya megawati 237, kwa hiyo megawati 32 hazizalishwi. Alifafanua jumla ya umeme ambao hauzalishwi kwa sababu ya ukame na matengenezo ni megawati 388 za umeme hadi kufikia 23 Novemba 2022.
Akieleza mipango ya muda mfupi ya kunusuru hali ya upungufu wa umeme, Bw. Chande alisema ni kuharakisha matengenezo ya mtambo katika kituo cha Ubungo III ili kuingiza megawati 35 za umeme hadi kufikia leo, kuharakisha matengenezo ya mitambo miwili ya Ubungo III ili kuingiza megawati 40 za umeme mwishoni mwa mwezi Disemba 2022.
Sambamba na kukamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kidatu ili kuingiza megawati 50 za umeme tarehe 30 Novemba 2022 pamoja na kuharakisha ufungaji wa mitambo miwili katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi I ili kuingiza megawati 90 za umeme kabla ya mwisho wa mwezi Disemba 2022.
“Iwapo matengenezo haya yatakamilika kama yalivyopangwa, yatatupatia jumla ya megawati 277 kwenye uzalishaji na kupunguza kadhia hii ya umeme,” alisisitiza Bw. Chande.
Aidha, Bw. Chande alisema juhudi za muda wa kati ni ukamilishaji wa ufungaji wa mtambo mwingine katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi I ili uanze kufanya kazi ili tuingize megawati 90 za umeme kwenye uzalishaji ifikapo mwezi Februari 2023 na kufikisha jumla ya megawati 337 za umeme.
Akihitimisha, Mkurugenzi Mtendaji alisema jitihada za muda mrefu ni kuharakisha ujenzi wa bwawa la Julius Nyerere.
“Hatua za muda mrefu ambazo ni zaidi ya miezi 12 mpaka 18, ni matumaini yetu, nguvu zetu na nia yetu bwawa la Julius Nyerere likamilike ili upungufu wa umeme uwe umekwisha” alihitimisha Bw. Chande.