Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema
Mkandarasi anaetekeleza mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) Mw 2115
ameshalipwa jumla ya shilingi trilioni 2.7 kulingana na mpango kazi kati
ya shilingi trilioni 6.5 anazotakiwa kulipwa hadi kukamilika kwa mradi.
Dkt. Mwinuka ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 03, 2021 katika ziara ya
Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais Ikulu na Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Kwa upande wake Karani wa Baraza la Mawaziri, Bw. Nsubili Joshua amesema
ameongozana na Maafisa wa Sekritarieti ili kujionea kazi inavyoendelea
JNHPP.
Amesema mradi wamekuwa wakiufahamu kwenye makaratasi hivyo wamefika kujionea hali halisi na kuona kinachoendelea.
Ameongeza kuwa wameona mambo makubwa ambayo hawayajatarajia na kutoa
pongezi kwa viongozi wakuu Serikalini kwa kuutekeleza mradi huo.
Awali akieleza lengo la ziara hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais
Menejimenti ya utumishi wa umma, Bw. Lauren Ndumbaru amesema wamefanya
ziara katika mradi na watumishi wa umma wa ngazi zote ili watumishi
waweze kuona na kuthamini kazi ambayo Serikali inafanya katika ujenzi wa
miradi ya kimkakati.
"Naamini kabisa mradi wa Julius Nyerere ukikamilika utaleta maendeleo
makubwa katika Nchi yetu, niombe watumishi wa umma wafanye kazi kwa bili
na waendelee kuiunga mkono Serikali ili tuone matokeo mapema" amesema
Bw. Ndumbalo
Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali amesema Wizara ya Nishati
imefarijika kutokana na Ofisi zote mbili kuridhishwa na utekelezaji wa
mradi wa Julius Nyerere.
"Tunamshukuru Rais Samia Hassan kwa kuendelea kuuangalia mradi huu kwa
jicho la kipekee kabisa, tunapata pesa za kuendeleza mradi kwa wakati na
usimamizi mzuri, tutaendelea kuusimamia na kuhakikisha mradi huu
unakamilika kwa wakati" amesema Bw. Mahimbila.
No comments:
Post a Comment