December 22, 2016

WANAKIJIJI WALIO KWENYE MRADI WA BACKBONE KUUNGANISHIWA UMEME KWA SHILINGI 27,000


Na Magreth Subi, Grace Kisyombe, Singida
WANAKIJIJI wa vijiji 126 wanaopitiwa na mradi mkubwa wa Umeme, Backbone wa Ujenzi wa Njia yaKkusafirisha Umeme wa Msongo wa Kilovolti 400, kutoka Mkoani Iringa hadi Shinyanga kupitia Mikoa ya Singida na Dodoma, wataunganishiwa Umeme kwa kulipia kiasi kidogo cha fedha shilingi elfu 27,000/-, tu, Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji, (pichani juu) amesema.
Bi. Leila ameyasema hayo kwenye Kijiji cha Igurubya, Mkoani Shinyanga, wakati wa Ziara ya Wahariri wa Vyombo vya Habari kutembelea mradi huo, Desemba 22, 2016.
“Nia ya Serikali, kupitia Shirika lake la Umeme Nchini TANESCO, ni kuwapatia Wananchi wote Huduma ya Umeme, ambayo ni muhimu katika kuinua Uchumi wa Mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla, kwa kawaida gharama ya kuunganishiwa Umeme kwa Vijijini ni shilingi 177,000/- pamoja na kodi ya ongezeko la thamani VAT.” Alisema.
Alisema, kwa kuzingatia hilo, kumekuwepo na juhudi mbalimbali za Shirika la Umeme, TANESCO, kufikisha Huduma ya Umeme Vijijini chini ya mradi wa Wakala wa Usamabzaji Umeme Vijijini (REA), lakini kukamilika kwa mradi huu wa Backbone kutaongeza kasi ya kuwapatia Wananchi Huduma hii muhimu ya Umeme na kwa bei nafuu.” Aliongeza.
 Alisema, Serikali kupitia TANESCO imepiga hatua kubwa ya kuwafikishia Umeme Wananchi ambapo tayari karibu asilimia 45 ya Wananchi wa Tanzania wamepatiwa Huduma ya Umeme.
Akizungumzia kukamilika kwa mradi huo wa Backbone uliojikita katika kujenga minara na njia za kusafirisha Umeme pamona na upanuzi wa Vituo vine vya kupoza na kusambaza Umeme, Meneja wa Mradi huo anayesimamia usafirishaji umeme, Mhandisi Oscar Kanyama, alisema, mradi huo wa Backbone wa kusafirisha Umeme wa msongo wa Kilovolti 400, na urefu wa Kilomita 670, kutoka Mkoani Iringa hadi Shinyanga kupitia Mikoa ya Singida na Dodoma, umekamilika rasmi Desemba 22, 2016 kwa kuwasha kipande kilichokuwa hakijakamilika cha kutoka Dodoma kwenda Singida.
Mradi huo ulianza kutekelezwa mwishoni mwa Mwezi Novemba mwaka 2013 na unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo umegharimu karibu shilingi Trilioni 1.
Kazi iliyokuwa ikifanywa ni pamoja na ujenzi wa minara mikubwa yenye uwezo wa kubeba nyaya 6, tatu kila upande tofauti na ile ya awali iliyokuwa na uwezo wa kubeba nyaya 2 tu moja kila upande. “Lakini pia kazi nyingine iliyokuwa ikifanyika chini ya mradi huu, ni upanuzi wa vituo vinne vya kupoza na kusambaza umeme, vituo hivyo ni kile cha Iringa, Zuzu, mkoani Dodoma, Kibaoni Mkoani Singida, na Ibadakuli Mkoani Shinyanga Shinyanga.” Alifafanua.

 Meneja wa Mradi huo anayesimamia usafirishaji umeme, Mhandisi Oscar Kanyama, akizungumza kwenye kituo cha Kibaoni Singida
 Mkuu wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Kibaoni mkoani Singida, akitoa maelezo kwa wahariri

 Mhariri wa Star TV, Jenifer Sumi
 Mhariri wa Clouds Media, Joyce Shebe, akinakili maelezo ya kiufundi kuhusiana na kituo cha umeme cha Kibaoni mkoani Singida.
 Picha ya pamoja ya wahariri na wafanyakazi wa TANESCO mkoani Sinfida
 Kituo cha Kibaoni mkoani Singida ambacho kilifanyiwa upanuzi chini ya mradi wa Backbone
 Mdhibiti mifumo ya umeme kituo cha Kibaoni Mkoani Singida, aimuonyesha kitu Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, na Katibu Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, (TEF), Neville Meena
 Minara ya kubeba nyaya za kusafirisha umeme, upande wa kulia ni minara mipya na kushoto ni ile ya zamani

December 21, 2016

ziara ya wahariri Dodoma na Singida



Mwendesha mifumo ya umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kituo cha kupoza na kusambaza umeme (Zuzu Sub-station), Bw. P.H. Rashid akitoa maelezo ya kiufundi kuhusu mabadiliko ya kimfumo yaliyoletwa na mradi wa Backbone wa ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha umeme kuanzia mkoani Iringa hadi Shinyanga kupitia mikoa ya Dodoma na Singida, wakati wahariri wa vyombo vya  habari walipotembelea kituo hicho. Mfumo huo mpya ambao uliwashwa kwa awamu Julai mwaka huu mkoani Iringa - Dodoma, utawashwa Desemba 21, 2016 kwa sehemu iliyobaki ya Shinyanga-Singida.
Wahariri wa vyombo vya  habari wakipatiwa maelezo ya kiufundi na wahandisi wa TANESCO kwenye kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu mkoani Dodoma ambacho kimepanuliwa chini ya mradi mkubwa wa umeme wa Backbone

Meneja Mradi mkubwa wa umeme wa Backbone, unaoendeshwa na serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania, (TANESCO), Mhandisi  Khalid James, (kulia), na Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji kituo cha kupoza umeme cha Kibaoni mkoani Singida wakati wa ziara ya wahariri vyombo vya  habari mkoani kutembelea mradi huo Desemba 20, 2016
Mdhibiti wa mifumo ya umeme kituo cha kupoza umeme cha Zuzu mkoani Dodoma, Bi. Itika Alexander, akiwa kazini wakati wahariri wa vyombo vya habari walipotembelea kituo hicho Desemba 20, 2016.
Minara mikubwa na ya kisasa ya kusafirisha umeme mkubwa (High tension), iliyojengwa chini ya mradi wa Backbone ikionekana kandokando ya barabara ya Dodoma-Singida
Mkuu wa kituo cha kupoza na kusafirisha umeme cha Zuzu mkoani Dodoma, Mhandisi, Joseph Mongi, akitoa maelezo ya kiufundi kuhusu hatua mpya iliyopigwa na TANESCO katika kuimarisha miundombinu ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400 wa Backbone kutoka mkoani Iringa hadi Shinyanga kupitia Dodoma na Singida.
Wahariri wakipatiwa maelezo
Kituo cha Zuzu cha kuposa na kusambaza umeme
Reactors mpya zilizojengwa kwenye kituo cha kupoza na kusafirisha umeme cha Zuzu mkoani Dodoma
Baadhi ya wahariri na afisa wa TANESCO kutoka kitengo cha Mahusiano, (kulia)
Kituo cha kupoza na kusambaza umeme cha Zuzu ambacho kimepanuliwa chini ya mradi wa Backbone

December 20, 2016

WAHARIRI WATEMBELE MARADI WA UFUAJI UMEME BACKBONE IRINGA-SHINYANGA.



 
Mhandisi Khalid James akizungumza na Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusu mradi wa ‘Backbone’, mradi unaounganisha mikoa ya Iringa, Dodoma, Singida na kuishia Shinyanga katika ofisi za TANESCO mkoani Iringa, jana. (Picha na Mpiga Picha Wetu)
 Na Magreth Subi, Grace Kisyombe

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), likishirikiana na vyombo mbalimbali vya habari nchini, limefanya ziara ya kutembelea mradi wa usambaziji wa umeme ‘Backbone’ unaoanzia Iringa na kuishia Shinyanga, mradi unaotarajia kuzinduliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, ili kujionea jidtihada za shirika hilo.

Mradi wa backbone unaanzia mkoani Iringa na kupita katika mikoa ya Dodoma, Singida na kuishia Shinyanga, ni mradi mkubwa unaoweka historia toka Tanzania imepata uhuru 1961. Akielezea mradi huo Meneja Mradi, kutoka TANESCO, Mhandisi Khalid Rueben James, alisema mradi huo utawanufaisha Watanzania kwa kupata umeme wa uhakika.

Mhandisi Khalid, alisema “mradi wa backbone utafanya ukarabati wa maeneo ya kupoozea umeme, pamoja na kunufaisha vijiji vilivyoko katika maeneo mradi unapopita.”  Mhandisi Khalid alieleza kuwa wananchi walioko katika vijiji hivyo watapata umeme kwa gharama nafuu kupitia mfuko wa uunganishwaji umeme vijijini (Rural Electrification Fund –REF)

Mhandisi Khalid alisisitiza kuwa vyanzo vingi vya umeme vinapatikana Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, ni pamoja na makaa ya mawe, joto ardhi, upepo  na maji kutoka katika bwawa la mtera. Aidha, alielezea   kwanini waliamua kuanzia mikoa inayo athirika kama Dodoma, Singida, Shinyanga ilikuondokana changamoto ya  kukatika umeme mara kwa mara.

Mhandisi Khalid alisema, mradi huu wa usafirishaji umeme ukikamilika utasaidia kuunganisha gridi ya taifa na gridi nyingine zikiwemo za mataifa jirani kama Kenya, Uganda, Ethiopia na Zambia.

Gharama za mradi wa backbone zimechangiwa na wahisani kutoka nchi mbalimbali ambao ni pamoja na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB), Shirika la Maendeleo Japan (JICA), Benki ya Uwekezaji ya Nchi za Ulaya (EIB), Shirika la Kiuchumi la Maendeleo Korea Kusini(EDCF), bila kusahau Serikali ya Jamuhuri ya Muungano Tanzania, Kwa ujumla gharama za  kukamilisha ujenzi wa mradi huu ni dola za  Marekani milioni 473.6

Mradi huu uliosimamiwa na Tanesco ulitekelezwa na wakandarasi ambao ni makampuni matatu ambayo ni KEC International Limimted, JYOTI Structures Ltd zote mbili kutoka India na GSE&C and Hyosung kutoka Korea Kusini. Ujenzi ulianza rasmi mwishoni mwa novemba 2013 na kukamilika kwa wakati ulipangwa kwa asilimia 100, alisema Muhandisi Khalid.

Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakimsikiliza Mhandisi Khalid James, walipotembelea kituo cha kupoozea umeme cha Tagamenda ambapo ndipo mradi wa Backbone unaanzia, mkoani Iringa jana. Mradi huo unaounganisha mikoa ya Dodoma, Singida na kuishia Shinyanga. (Picha na Mpiga Picha Wetu)

Minara mikubwa ‘Cross Sectional  Tower’ ya umeme yenye urefu wa mita 89.5 na umbali wa kilomita 1.6 kutoka mnara mmoja hadi mwingine katika bwawa la Mtera ni minara mirefu kuliko yote nchini, kama inavyoonekana katika picha. Minara hii ni sehemu ya mradi wa ‘Backbone’ mradi unaounganisha mikoa ya Dodoma, Singida na kuishia Shinyanga. (Picha na Mpiga Picha Wetu)