Na Henry Kilasila
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard
Matogolo Kalemani, amekagua Miradi ya uboreshaji wa Miundombini ya Umeme Jijini
Dar es Salaam, inayofadhiliwa na Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo
la Japan (JICA).
Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kukagua vituo vya
kupoza na kusambaza umeme vya Ilala, City Center, Muhimbili, Masaki na Msasani
iwapo vimekamilika na vinafanya kazi vizuri, ambapo aliridhishwa na vituo
hivyo.
Aidha, Dkt. Kalemani aliipongeza Menejimenti ya
TANESCO, Uongozi wa Kanda, Mkoa na Wafanyakazi kwa kuwezesha upatikanaji wa
umeme wa uhakika katika Hospitali ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo, Chuo cha
Muhimbili na Hospitali ya Mwananyamala ambapo kila moja imejengewa njia ya
umeme ya msongo wa Kilovolti 11 hivyo kuondoa matatizo ya umeme katika maeneo
hayo.
“Mahitaji ya Muhimbili ni Megawati 4 wakati kituo
cha Muhimbili kinamegawati 12, mahitaji ya Hospitali ya Mwananyamala ni
Megawati 1.5 wakati kituo kina Megawati 12, hivyo sitegemei kusikia umeme
umekatika katika maeneo haya”. Alisema Dkt. Kalemani na kuutaka Uongozi wa
TANESCO kuvisimamia vizuri vituo hivyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugrnzi Mtendaji TANESCO
Dkt. Tito E. Mwinuka alisema, Serikali iliona uwepo mkubwa wa mahitaji ya
umeme, hivyo kupitia TANESCO iliamua kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika
maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na kuviongezea uwezo Vituo vya kupoza
na kusambaza umeme, uboreshaji wa vyumba vya kuendeshea mitambo pamoja na
uboreshaji wa njia za kusafirisha umeme.
“TANESCO tunafanya jitihada za kuendelea kukamilisha
Miradi ambayo haijakamilika ya Mbagala na Kurasini, kwani Miradi hiyo ikikamilika
maeneo ya Kigamboni yatapata umeme wa uhakika hivyo mji wote wa Dar es Salaam
kuwa na umeme wa uhakika.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri pia alitembelea Chuo
cha Ufundi TANESCO cha Masaki eneo ambalo Wanafunzi wanafanya Mafunzo kwa
vitendo na kutoa pongezi kwa TANESCO na kuutaka Uongozi kuongeza idadi ya
Wanachuo.
Serikali kupitia TANESCO imeendelea na uboreshaji wa
Miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam ambapo kwa Kituo cha kupoza na
kusambaza umeme cha Ilala kimeongezwa uwezo kutoka MVA 210 hadi MVA 240, ujenzi
wa chumba kipya cha kuongezea mitambo na kujenga njia ya kusafirisha umeme ya
msongo wa kilovolti 132 kutoka Ubungo hadi Ilala.
Pia ujenzi wa njia ya usafirishaji wa umeme kupitia
chini ya ardhi ya msongo wa Kilovolti 33 katika Vituo vya City Center, Sokoine,
Railway na Kariakoo.
No comments:
Post a Comment