WAHANDISI na Mafundi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),
wanapambana usiku na mchana kuzifanyia matengenezo mashine za kufua umeme, ili
kuondoa tatizo la kukosekana kwa umeme kwa vipindi virefu kila siku kwenye Mikoa
ya Mtwara na Lindi.
Akizungumza mjini Mtwara Oktoba 14, 2017, Naibu
Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji, Mhandisi Kaitwa Bashaija, amesema kwa sasa
Wahandisi na Mafundi wa TANESCO wamekuwa wakifanya kazi usiku na mchana ili
kutengeneza mitambo ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.
Baadhi ya Wananchi wameshuhudia mafundi hao wakifanyakazi ya
kurekebisha mitambo hiyo katika Kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi
asilia Mkoani Mtwara.
“Mitambo hii ina kiasi cha mika 10 tangu ifungwe, na kadiri
miaka inavyokweda ndivyo ongezeko la uhitaji wa umeme hususan Mkoani Mtwara
linazidi kuongezeka kutokana na kukua kwa shughuli za kiuchumi,” Alisema
Mhandisi Bashaija.
Aliongeza, miaka michache iliyopita baadhi ya mitambo
iliweza kuzimwa na bado hali ya umeme ilikuwa imara.
Wiki iliyopita Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani
aliagiza TANESCO kufanya juhudi za ziada kuhakikisha tatizo la umeme mkoani
Mtwara na Lindi linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Kutokana na hali hiyo Mhandisi Bashaija, alisema kuwa kwa
sasa TANESCO winamipango ya muda mfupi na mrefu katika kuhakikisha miundombinu
ya umeme katika Mikoa ya kusini inaimarika.
Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme kwa
kutumia gesi asilia cha Mtwara, Mhandisi Mkulungwa Chinumba, alisema licha ya
changamoto hiyo kwa sasa bado mitambo iliyopo ina uwezo mkubwa wa kuzalisha
umeme katika Mikoa hiyo.
“Pamoja na hali hii lakini kwa sasa tunakwenda vizuri kiasi
ila si sana maana umeme kuna wakati unarudi na kukatika. Na tunaamini
tutafanikiwa kurudi katika hali ya kawaida na kikubwa tunawaomba Wananchi wa Mikoa
ya Mtwara na Lindi kutuvumilia kwani nasi tunajua umuhimu wa umeme katika
shughuli za uzalishaji.” Alitoa rai Mhandisi Chinumba.
No comments:
Post a Comment