|
Mafundi wakiwa wamebeba nondo wakati kazi ya ujenzi wa njia ya ardhi ya kuchepusha maji (dirvesion tunnel) ikiendelea. |
HATUA zote nane (8) za utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa
bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere (JNHPP-MW2115) kwenye
bonde la mto Rufiji unaendelea kwa kasi inayohitajika, Mhandisi mkazi wa
mradi huo Eng. Mushubila Kamuhabwa amewaambia waandishi wa habari
kwenye eneo la mradi Julai 17, 2020.
Eng. Kamuhabwa ametaja hatua hizo kuwa ni ujenzi wa njia kubwa ya
ardhini ya mchepuko wa maji (diversion tunnel), sehemu ya kufua umeme
(power house), ukuta utakaotengeneza bwawa, eneo la kupokelea umeme
unapozalishwa (Switch yard), power intake, barabara na madaraja, saddle
dams nne na kuchakata mawe yanayotumika kutengeneza zege na mahitaji
mengine.
“Mradi huu wa JNHPP una miradi mingi ndani yake na yote iko katika hatua
mbalimbali na hatua hizo kama nilivyozitaja kwa pamoja ndiyo zinajenga
mradi mmoja wa Julius Nyerere Hydro Power Project Megawati 2115 katika
hilo ujenzi unaendelea katika maeneo yote hayo, mafundi wako kazini na
wanaendelea na ujenzi kwa kasi kubwa kama inavyohitajika.” Alisema Eng.
Kamuhabwa.
Alisema jambo la kufurahisha tayari mradi umeanza kuchangamsha uchumi wa
nchi na kutolea mfano wakati wakiweka zege kwenye njia ya kuchepusha
maji (diversion tunnel, zaidi ya tani 200 za nondo zimetumika hii
inafaidisha viwanda vyetu hapa nchini lakini pia wananchi wanaokaa
vijiji vinavyozunguka eneo la mradi wanafaidika kwa namna mbalimbali
ikiwwemo miundombinu wezeshi kama vile umeme unaotoka Morogoro kuja hapa
umepitia kwenye vijiji kadhaa natayari baadhi yao wameanza kufaidika na
umeme huo.” Alisema na kuongeza…Lingine zaidi ya vijana wa Kitanzania
wapatao 4,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini hususan yale yanayozunguka
eneo la mradi wameajiriwa na wanashiriki katika mradi kwa ari kubwa.
“Tunatarajia idadi hiyo ya ajira ikaongezeka hadi kufikia watu 6,000
mradi utakapofikia hatua ya juu peak.” Alisema Eng. Kamuhabwa.
Kwa upande wao baadhi ya wanakijiji wa Kisaki kilomita 60 kutoka eneo la
mradi wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Magufuli kwa kuwaletea mradi huo kwani tayari manufaa yake wameanza
kuyaona.
“Kisaki inakuja juu, tuna uhakika mradi ukimalizika Kisaki itakuwa kama
Morogoro, kwa sasa biashara inakuwa kwa kasi sana tofauti na hapo awali,
mfano mchele tunauza kwa kilo shilingi 1,600/= tofauti na hapo awali
tulikuwa tunauza shilingi 500/= bei ya juu kabisa shilingi 1,000/=, watu
wameongezeka sana.” Alisema mwanakijiji wa Kisaki Ali Matumbo na
kuongeza…umeme nao tayari umefika kijijini kwetu, shule imepata umeme
kwa hivyo tunafuraha sana kwa ujio wa mradi huu na tunampongeza sana
Rais wetu Magufuli.
Naye mwanakijiji mwingine Bi. Asha Said alisema, anauhakika hata
barabara nzuri itajengwa kutokana na mradi huo na anafurahi kuona wageni
wengi wanafika Kisaki na hivyo biashara zao zimechangamka.
Naye mwanakijiji mwingine Hassan Mohammed Ngozi alisema, anayo matumaini
makubwa kwa hali anavyoiona hivi sasa hapo Kisaki, mradi
utakapokamilika watakuwa na Kisaki mpya.
“Kwetu sisi ongezeko la watu hapa Kisaki limekuwa na faida
kubwa………..watu wakienda kufanya kazi huko kwenye mradi wanakuja hapa
kijijini wananunua bidhaa zetu na sisi tunapata pesa haya ni manufaa
makubwa kwetu.” Alisema Bw. Ngozi.
|
Mhandisi Mkazi wa Mradi wa Julius Nyerere, Mhandisi Mushubila Kamuhabwa akizungumza na Waandishi wa Habari eneo la Mradi. |
|
MAshine zikichoronga miamba ya ardhi ili kutengeneza njia ya kuweka baruti kwa ajili ya kulipua miamba hivyo kuhamisha milima |