August 18, 2021

Hatua nyingine kubwa JNHPP

 

Kazi ya usimikaji wa bomba (Draft tube) sehemu ya chini kabisa kwenye mashine nambari 9 imeanza Agosti 17, 2021, katika mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), bomba hizo zitatumika kutolea maji katika mitambo ya kufua umeme na kuyarudisha mto Rufiji kwa ajili ya matumizi mengine.

Hii ni hatua kubwa iliyofikiwa baada ya kukamilika kwa uundwaji wa bomba hizi zinazofungwa katika kitako cha msingi wa zege, kilichopo eneo la mita 42.7 juu ya usawa wa bahari.

Usimikaji wa bomba hizi ndio utawezesha kuanza kwa ufungaji wa sehemu za juu za mashine (turbine) na kisha jenereta za kufua umeme.

 




 

August 14, 2021

WAZIRI MKUU AKAGUA KITUO CHA TANESCO MSAMVU BAADA YA KUATHIRIKA NA MOTO

 

Waziri Mkuu wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, leo Agosti 14, 2021 amekagua kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro.

Mhe. Majaliwa amekagua athari zilizotokea baada ya kupata hitilafu iliyopelekea kuwaka moto kwa jumba la kudhibiti mifumo ya umeme wa msongo wa kilovolti 33 Agost 2, 2021.

Aidha, amewataka Wafanyakazi wa TANESCO kuendelea kufanya kazi kwa uaminifu na weledi kutokana na nishati ya umeme kuwa ndio injini ya ukuaji uchumi wa Nchi.

" Watumishi wa TANESCO mmebeba mioyo ya watu, muongeze umakini katika utendaji wenu wa kazi", amesema Mhe. Majaliwa.

Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa ameiagiza TANESCO Kufanya mapitio ya Wafanyakazi wanaosimamia vituo vya kupokea na kupoza umeme ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi.

Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro ni moja kati ya vituo 51 ambavyo vinapokea na kupoza umeme mkubwa wa gridi ya Taifa.

 





 

August 11, 2021

NAIBU KATIBU MKUU AKAGUA MRADI YA UMEME LUGURUNI

 


Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali, Agosti 07, 2021 alikagua utekelezaji wa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Luguruni Jijini Dar es Salaam.

Utekelezaji wa mradi wa Luguruni ulianza Aprili 01, 2020 na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2021 ikiwa ni miezi 18 ya utekelezaji wa mradi.

Kukamilika kwa mradi wa Luguruni kutaboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mikoa wa Pwani na Dar es salaam hasa kwa maeneo ya Kimara, Mbezi, Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, msigani, kibamba, kibwegere, kisarawe, Maili moja na TAMCO (Industrial area) ambayo yamekuwa na changamoto ya kukosekana kwa umeme wa uhakika kutokana na njia za umeme zinanipeleka maeneo hayo kusafiri umbali mrefu.

Gharama za uzalishaji mradi wa Luguruni ni Shilingi Bilioni 15.2 ambazo zinagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 





MANUFAA YA KITUO CHA UMEME DEGE KWA KIGAMBONI NA MAENEO YA JIRANI


 Kituo cha kupokea na kupoza umeme  cha Dege ni mkombozi katika kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Wilaya ya Kigamboni na maeneo jirani kutokana na kuimarisha upatikanaji wa umeme baada ya  kukamilika kwa utekelezaji wake Aprili 30, 2021.

Maeneo ya Viwandani, Pemba Mnazi, Mwasonga, Mwongozo, Kimbiji na maeneo jirani awali yalikuwa yanapata changamoto ya umeme kukatika au kuwa mdogo kutokana na njia ya umeme kusafiri umbali mrefu kutokea Mkoa wa kitanesco wa Ilala.

Akitembelea kituo hicho Agosti 07, 2021 Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali ameridhishwa na usimamizi wa kituo cha Dege ambacho kilianza kujengwa Mei 02, 2019.

Aidha, mahitaji ya sasa ya Wilaya ya Kigamboni ni megawati 18 huku uwezo wa kituo cha Dege ni megawati 48 lakini malengo ya Serikali ni kukiongezea uwezo hadi hadi kufikia megawati 96.

 




 

August 10, 2021

TANESCO NA STAMICO WASAINI UTEKELEZAJI MRADI WA MAKAA YA MAWE KIWIRA

 


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Agosti 10, 2021, limesaini hati ya makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhusu utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kwa kutumia makaa ya mawe ya Kiwira.

Akiongea wakati wa uwekaji saini Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema utekelezaji wa mradi wa Kiwira utaenda sambamba na ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka ya urefu wa km 100 kutoka Kiwira hadi kituo cha kupokea umeme cha Mwakibete Mbeya.

Aliongeza kuwa, kwasababu mradi unagusa Taasisi mbili ni vyema kuwa na hati ya makubaliano ili kufahamu jukumu la kila Taasisi.

"STAMICO na TANESCO ni wadau wa mradi wa Kiwira, kwa maana kwamba STAMICO wao wanahusika na mgodi wa makaa ya mawe, TANESCO tutasimamia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme", alisema Dkt. Mwinuka.

Amesema utekelezaji wa mradi wa Kiwira umeambatana na faida nyingi kwa Nchi ikiwemo uwepo umeme wa kutosha na kuweza kufanya biashara na Nchi jirani.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji STAMICO, Dkt. Venance Mwase amesema jukumu kubwa la STAMICO ni uchimbaji wa madini.

Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa Taasisi za Serikali kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo na hata kutoa huduma.

"Siku hii ya leo tumefikia makubaliano na TANESCO katika kuuendeleza mradi wa Kiwira kwa manufaa ya Taifa ", alisema Dkt. Mwase.