December 2, 2010

Kamati za Wahandisi zazinduliwa upya

Picha ya pamoja ya wajumbe wa kamati za wahandisi za Shirika la Umeme Tanzania - TANESCO.

Kamati za wahandisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) zilizokuwepo kabla ya utawala wa Net Group Solutions zimezinduliwa upya hivi karibuni chini ya Mwenyekiti wake Mhandisi Stephen Mabada ambaye pia ni Meneja Mkuu Ufuaji Umeme.

Kamati hizo zinahusisha wahandisi wa fani zote ndani ya Shirika na zina jumla ya wajumbe 24.
Mhandisi Mabada akisoma risala kwa niaba ya mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika Mhandisi William Mhando.

Katika risala yake, Mhandisi Mhando aliwashukuru wajumbe wa Kamati hizo kwa kurejesha tena vikao hivyo ambavyo ni vya juu kabisa vya masuala ya kihandisi ndani ya Shirika.

Mhandisi Mhando alisema atatoa kipaumbele cha kwanza kwa wahandisi kwani ndio msingi wa shughuli kuu za Shirika letu lakini bila kusahau fani nyingine ndani ya shirika.

Akirejea mwito wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Bw.David Jairo kwenye Baraza Kuu la Wafanyakazi wa TANESCO lililomalizika hivi karibuni, alisema wahandisi inabidi wapewe kipaumbele ili kufikia malengo ya Shirika.

Mhandisi Mhando pia kwenye risala yake alisema Shirika lina matatizo mengi yanayohitaji wahandisi akitaja tatizo la kufua umeme kwa gharama kubwa na viwango vidogo, upotevu wa umeme wakati wa usafirishaji na usambazaji, wingi wa ajali zitokanazo na kazi za kihandisi na wizi wa miundombinu mbalimbali ya Shirika.
Risala yake pia ilisisitiza matarajio yake kuwa kamati hizo za kihandisi zitasadia kutatua matatizo hayo ya kihandisi na hatasita kuwazawadia wahandisi ambao ubunifu wao utaleta mafanikio katika kutatua matatizo hayo na ubunifu pia wao utapunguza gharama za kutumia washauri kutoka nje ya Shirika.

Shirika la Umeme TANESCO kwa sasa lina jumla ya wahandisi 338 licha ya kuwa zipo sehemu mbalimbali ambazo bado zinahitaji wahandisi, idadi hii ni hazina kubwa kwa Shirika. 

1 comment:

  1. karibu kwenye ulimwengu wa blogu! duhu kazi mnayo ya kukutana na changamoto za matusi na kero za umeme wa Bongo. mimi niko Bukoba umeme ni wa Ugandaaaa! taitizo mvua kidogo umeme wakatika sijui radi!

    ReplyDelete