June 25, 2014

Kutoka kwa grid

Jana  majira ya saa 1.19 usiku gridi ya taifa ilitoka na hivyo kusabisha nchi nzima kikosa umeme. Umeme ulirejeshwa kwa nchi nzima saa 4:48 usiku baada ya kuwasha mashine zote bila tatizo kuonekana.Kutoka kwa gridi ya taifa kuna sababu mbili kuu: Moja kama kukitokea hitilafu , mmoja wa mitambo yetu ya kuzalisha umeme mfano: Kidatu, Mtera, Kihansi, Hale, New Pangani, Nyumba ya Mungu, Ubungo 1&2 au Tegeta gridi inaweza kutoka. Yaani kwa lugha rahisi ni kwamba mitambo yote ya kuzalisha umeme inabeba mzigo mmoja. Kama mtambo mmoja ukitoka, unasababisha ombwe (vacancy) ambapo mitambo inayobaki inashindwa kuubeba na hivyo nayo kuachia mzigo na hatimaye mashine zote hutoka (huzima). Sababu ya pili mitambo ya wateja wetu wakubwa kama vile, migodi na viwanda vikubwa vya uzalishaji, wateja hao wakubwa mitambo yao ikipata hitilafu na kuzima ghafla, inaweza kusababisha mfumo wa gridi kutoka kwa mtindo huo huo wa kuzidiwa kwa mzigo kwa mitambo yetu. Hivyo baada ya gridi kutoka mafundi kwenye vituo vyetu wakishirikiana na kituo cha kudhibiti mifumo ya gridi waliweza kuwasha mashine zote salama na umeme kurejeshwa nchi nzima saa 4.48. Kwa hivyo mpaka sasa bado tunafanyia kazi taarifa/data zilizorekodiwa na Kituo cha kudhibiti mifumo cha Ubungo ilikujua haswa chanzo cha kutoka kwa gridi jana usiku. Kitendo cha jana tutkichukulia kua ni dharura na ghafla (emergency) ni nadra sana kutokea gridi yote kutoka.
Kwa nchi za wenzetu gridi haiwezi kutoka kwa kuwa wanazalisha umeme wa ziada (spinning reserve) kwa kuwa wanazalisha umeme kwa njia kama ya makaa ya mawe ambao ukishauwasha huwezi kuuzima, hivyo wanaumeme ambao uko standby, ukipungua tu kwenye gridi basi spinning reserve inaziba hilo ombwe.

Adrian Severin - Kaimu Meneja Uhusiano Tanesco

No comments:

Post a Comment