June 5, 2014

TAARIFA KWA UMMA

                                             SHIRIKA LA UMEME TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU UPOTOSHAJI WA GAZETI LA MTANZANIA

Gazeti la Mtanzania la Mei 30, 2014 toleo namba 7476 lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari “ Vigogo TANESCO wadaiwa kutafuna Sh milioni 408” kwenye ukurasa wa tisa na gazeti hilo hilo la Juni 4, 2014 toleo namba 7481 lilichapisha tena mwendelezo wa taarifa hiyo ikiwa na kichwa cha habari “Vigogo TANESCO watoa vitisho”.

Taarifa hiyo inalishutumu Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa limekumbwa na kashfa nyingine kwa madai kwamba viongozi kadhaa wa Shirika wamekula kiasi hicho cha fedha, ambazo ni posho za wafanyakazi 36 kutoka mkoa wa Dar es Salaam.
Uongozi wa TANESCO unakanusha vikali taarifa hizo na kwamba hazina ukweli wowote.

Kwanza taarifa hiyo inamakosa mengi ya kiuandishi. TANESCO ina makubaliano na Shiririka la Maendeleo la Watu wa Japani (JICA) kuwafundisha wafanyakazi wake kwenye mpango ujulikanao kama ““Capacity Development of Efficient Distribution and Transmission Systems” yaliyosainiwa mwaka 2009. Hakuna Kampuni inayoitwa Jaica inayofanyakazi na Shirika kama mwandishi alivyoandika kwenye habari zake zote mbili.

Pili katika makubaliano hayo, JICA wanachangia wataalamu na vifaa vya kufundishia kwa njia ya vitendo na nadharia wakati TANESCO walichangia ujenzi wa majengo na wanaendelea kulipia posho za wafanyakazi wanafunzi katika vyuo vyake viwili vilivyopo jijini Dar es Salaam eneo la Masaki na Stesheni.

Wanaofundishwa chini ya mradi huu ni wafanyakazi  ambao ni mafundi yaani mafundi sadifu, mafundi mchundo na wahandisi. Mradi huu ambao unafundishwa kwa pamoja na wataalamu kutoka TANESCO na JICA (Japan) unategemewa kukamilika Agosti mwaka huu na baadae, TANESCO wataendelea kutoa mafunzo hayo kwa mtindo ambao wameuanzisha pamoja na JICA.

Tatu, mapungufu ya taarifa hiyo
Mwandishi wa taarifa hiyo alikuwa na ufahamu mdogo wa mpango wenyewe. Ukweli ni kwamba Mradi una taratibu mbili za ufundishwaji. Kundi la kwanza ni ufundishaji wa wafanyakazi wanaopewa mafunzo ya darasani kwa nadharia na kwa vitendo ndani ya maeneo ya Chuo na wamatoka mikoani. Kundi ya pili ni wafanyakazi mafundi wanaopewa mafunzo ya vitendo tu kwenye miundombinu ya Shirika iliyopo baada ya kumaliza mafunzo ya awali kwenye maeneo ya Chuo. Mafunzo haya yanajulikana kama ‘On Job Training’ (OJT). 

Wafanyakazi wanaodaiwa kulalamika ni wanaofanya mafunzo kwa vitendo wakati wakiwa kazini (OJT) nje ya Chuo na wamepewa kazi ya kuboresha miundombinu ya umeme katika jiji la Dar es Salaam na wanatoka mikoa ya Kinondoni Kaskazini (Mikocheni), Kinondoni Kusini (Magomeni) na Kituo cha Karabati Umeme Dar es Salaam (KAUDA).

Mradi wa kuboresha miundombinu kwa mkoa wa Dar es Salaam ili kuondokana na kukatika katika kwa umeme ulianza mwaka 2009 kwa ushirikiano kati ya JICA na TANESCO nia ya mpango huu ilikuwa ni kujenga uelewa wa kiufundi zaidi baada ya mafunzo ya darasani ambapo mafundi hupelekwa maeneo yao ya kazi kufanyakazi kwa vitendo.

Nne, Utaratibu wa Shirika
Kulingana na taratibu za Shirika na Sheria za kazi, TANESCO hutoa posho ya siku kwa wafanyakazi wanaohudhuria mafunzo ya darasani yakiandamana na vitendo vinavyofanywa ndani ya eneo la Chuo Masaki. Lakini hawa wafanyakazi wanaolalamika kwa mujibu wa kumbukumbu za Shirika hawatambuliki kama wanafunzi tena. Walishamaliza mafunzo ya darasani na ya vitendo katika eneo la Chuo lilipo Masaki jijini Dar es Salaam na wakalipwa posho kwa mujibu wa taratibu na sasa wapo mitaani wanatekeleza yale waliyojifunza darasani. Hawa ni wafanyakazi kama wafanyakazi wengine na wanapokea misharara yao na marupurupu mengine yote kila mwisho wa mwezi.

Kwa jinsi Shirika linavyowajali na kutambua kazi wanayoifanya, licha ya mishahara yao na marupurupu mengine, wakati huu wanapofanya kazi kwa vitendo wakati wapo kazini (OJT) kwenye Mpango huo maalum wa kuboresha mifumo ya usambazaji umeme kwa jiji la Dar es Salaam, wanalipwa kiasi cha fedha kama motisha kutoka kwenye vituo vyao vya kazi kwa kupimwa kupitia malengo waliyoyafikia kwenye (OJT).

Tano, mwendelezo wa habari hiyo
Kama vile haitoshi, gazeti hilo limeiendeleza habari hiyo kama vile ina ukweli wowote na mbaya zaidi gazeti hilo halijafanya jitihada zozote za kutafuta ukweli kutoka TANESCO. Aidha linadai kuwa wafanyakazi hao wanatishiwa, sababu ambayo haina msingi wowote.

Mwisho. Uongozi wa Shirika umesikitishwa kwa taarifa hizo ambazo zimechafua taswira ya Shirika na linautaka uongozi wa Gazeti la Mtanzania kwa ajili ya kuendeleza Uhusiano mzuri uliopo baina ya Shirika na vyombo vya habari kukanusha taarifa hizo kwenye gazeti hilo hilo na kuuomba radhi uongozi wa TANESCO kwa udhalilishaji ambao umepotosha umma.

Imetolewa na:  Ofisi ya Uhusiano,
TANESCO Makao Makuu.

No comments:

Post a Comment