August 28, 2018

TANESCO YAZALISHA UMEME WA KUTOSHA


Imebainishwa kuwa Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO) kwa sasa linazalisha umeme wa kutosha mahitaji ya nchi huku ziada ikiwa ni zaidi ya megawati 200 na hivyo kupelekea kupungua kwa changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi  Mtendaji wa TANESCO,  Dkt. Tito Mwinuka,  leo tarehe 28/08/2018 wakati akiwasilisha Taarifa ya Shirika hilo kwa Kamati  ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Ameeleza kuwa, umeme unaozalishwa sasa ni takribani megawati 1517.47 huku matumizi yakiwa ni takribani ni megawati 900.

Aidha, Dkt. Mwinuka ameeleza kuwa Shirika hilo linaendelea na juhudi za kuwaunganishia umeme wananchi, kazi ambayo inaenda  sambamba na kuimarisha mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kupunguza  matukio ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Ameeleza kuwa, kutokana na jitihada hizo, mapato ya Shirika yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kuliwezesha Shirika kujiendesha bila kutegemea ruzuku kutoka serikalini tangu mwaka 2015/16.

“Mapato ya Shirika yameendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha mwaka 2017/18, makusanyo yamekuwa ya wastani wa  shilingi bilioni 38 hadi 39 kwa Wiki kutoka wastani wa shilingi bilioni  34 katika mwezi Aprili, 2018,” amesema Dkt. Tito Mwinuka.

Akizungumzia suala la deni la TANESCO, Dkt. Mwinuka amesema kuwa  kuna sababu mbalimbali zinazopelekea deni la Shirika kuongezeka ikiwa ni pamoja na gharama kubwa za uzalishaji wa umeme katika maeneo yaliyopo mbali na gridi ya Taifa ambapo TANESCO hulazimika kuzalisha umeme kwa wastani wa shilingi 763 kwa uniti moja.

Akizungumzia mikakati ya Shirika katika kulipa madeni kwa wadai wake, Dkt.  Mwinuka alisema kuwa wameweka mipango mahsusi ili kulipa gharama hizo kila mwezi ili deni lisiendelee kukua, kuwalipa deni lote wadai wadogowadogo kwa wakati na kujadiliana na wadai ili kuondoa riba.

Aliongeza kuwa,  juhudi nyingine zinazofanywa na TANESCO ili kupunguza madeni kwa Shirika ni  kutafuta mikopo yenye masharti nafuu,  kuongeza na mapato.


No comments:

Post a Comment