December 3, 2014

TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUKOSEKANA KWA UMEME KWA BAADHI YA MAENEO KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAMShirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linanapenda kutoa ufafanuzi kwa wateja wake kuhusu kukosekana kwa umeme kwa baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali kama ifuatavyo:-

Mosi, Kuanzia Novemba 26, 2014 hadi Desemba 1, 2014 Mikoa yote iliyoungwa kwenye gridi ya taifa ikiwemo Dar es Salaam ilikuwa na upungufu wa umeme kwa baadhi ya maeneo kutokana na kuharibika kwa mashine moja ya Mtambo wa Kufua Umeme wa Kidatu yenye uwezo wa kufua megawati 50. Mtambo huo kwa sasa umetengamaa na hakuna Mkoa wenye upungufu wa umeme.

Pili, Novemba 29, 2014 Kulitokea hitilafu ya kuungua kwa Kikata Umeme (Circuit Breaker) kwenye Kituo cha Kupooza na Kusambaza Umeme cha Ubungo upande wa msongo wa kilovolti 33 na hivyo kusababisha baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Kinondoni Kusini (Magomeni) kukosa umeme kwa siku 2 mfululizo. Tatizo hilo limeshapatiwa ufumbuzi na Mkoa huo kwa sasa unapata umeme kama kawaida.

Tatu, Kuanguka kwa nguzo kwa baadhi ya maeneo katika jiji la Dar es Salaam kutokana na kuanza kwa kipindi cha mvua.

Nne, Matengenezo yanayoendelea ya ukarabati wa miundombinu kwa mikoa yote ya Dar es Salaam. TANESCO inaendesha zoezi la ukarabati wa miundombinu yake kwa mikoa ya Kinondoni Kusini (Magomeni), Kinondoni Kaskazini (Mikocheni), Ilala na Temeke. Kazi zinazofanyika kwenye zoezi hilo kwa sasa ni kubadilisha nguzo zilizooza, kunyanyua nguzo zilizoinama, kuvuta nyaya zilizolegea na kukata miti inayogusa nyaya za umeme. Zoezi kama hili hufanyika kwa kila mkoa kwa nchi nzima kama tahadhari kabla ya kuanza kwa kipindi cha masika ambacho kinaambatana na mvua na upepo mkali.

Kwa sababu hii kubwa, kumekuwa na usumbufu wa kukatwa kwa umeme kwa baadhi ya maeneo mara moja kwa siku ili kupisha zoezi hilo ambalo tunatarajia litakamilika mwezi huu wa Desemba.

Uongozi wa Shirika unaomba radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza.

Imetolewa na
Ofisi ya Uhusiano,
TANESCO MAKAO MAKUU.

No comments:

Post a Comment