February 29, 2016

UFAFANUZI JUU YA TAARIFA ZILIZOTOLEWA NA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU OMBI LA TANESCO KUSHUSHA BEI YA UMEMEUFAFANUZI JUU YA TAARIFA ZILIZOTOLEWA NA BAADHI YA VYOMBO
VYA HABARI KUHUSU OMBI LA TANESCO KUSHUSHA BEI YA UMEME

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limewasilisha ombi la kushusha bei ya umeme kwa asilimia 1.1 kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) pamoja na kuondoa kabisa gharama ya maombi ya awali kwa wateja wapya (gharama za Fomu) ya Shilingi 5,000 na gharama za huduma (service charge) ya Shilingi 5,520 kwa mwezi kwa wateja wote wa majumbani.

Maombi hayo yamewasilishwa baada ya TANESCO kufanya tathmini ya kina ya kimahesabu pamoja na kubuni namna ambayo wateja wake wanaweza kupata ahueni ya gharama kwa kuzingatia mazingira ya sasa.

Hata hivyo baadhi ya vyombo vya habari vimepotosha ukweli huo hivyo TANESCO inapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
Mosi, Kwa mujibu wa sheria, TANESCO inapotaka kubadilisha bei za umeme, iwe kushusha au kupandisha ni lazima iwasilishe maombi hayo EWURA kwa kuwa ndiyo mwenye mamlaka ya kisheria ya kubadilisha bei za umeme.

Pili, TANESCO huwasilisha maombi yake pamoja na takwimu halisi zinazoshawishi mantiki ya kubadilishwa kwa bei hizo na kwa maombi yaliyowasilishwa EWURA Februari 24, 2016 ndivyo TANESCO ilivyofanya.

Tatu, Baadhi ya mambo muhimu yanayoendana na mazingira ya sasa ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa gesi tofauti na ilivyokuwa hapo kabla na pia kuongezeka kwa ujazo wa maji katika mabwawa hasa Mtera.

Nne, japokuwa kiasi cha madeni kilichotajwa na vyombo vya habari sio sahihi, madeni hayo yamezingatiwa kikamilifu katika mapendekezo haya ya kushusha bei, hivyo si kweli kwamba kwa kushusha huko bei TANESCO itafilisika.

Aidha, kusema kwamba Serikali inailazimisha TANESCO kushusha bei ya umeme na kwamba kwa kufanya hivyo Shirika litafilisika sio sahihi hata kidogo kwani tathmini ya kitaalamu imefanyika na pia kwa mujibu wa sheria EWURA itafanya tathmini yake kabla ya kuidhinisha bei mpya.

Ieleweke kwamba Serikali ya awamu ya Tano imeshatoa fedha nyingi za kusaidia miradi ya umeme zikiwepo zaidi ya Shilingi Bilioni 100 zilizotolewa hivi karibuni kwa maelekezo ya Mh. Rais kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa Mradi mkubwa wa Kinyerezi II unaotekelezwa na Kampuni ya SUMITOMO ya Japan.

Pia Serikali imeendelea kulipa madeni ya umeme ya taasisi zake na hadi sasa sehemu kubwa ya madeni ya taasisi za Serikali yamelipwa.

Hivyo, TANESCO inaishukuru Serikali kwa jitihada kubwa inazozifanya katika kushughulikia changamoto za umeme nchini.

Imetolewa na:  Ofisi ya Uhusiano,
                         TANESCO Makao Makuu.

No comments:

Post a Comment