July 15, 2018

"TANESCO Changamkieni fursa" Naibu Waziri Nishati


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Iputi, Kata ya Mbuga, Wilayani Ulanga, akiwa katika ziara ya kazi Mkoani Morogoro,


Na Veronica Simba – Ulanga

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Subira Mgalu amewataka watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa wabunifu na kuzitumia vema fursa za kibiashara zinazojitokeza kwa kupeleka umeme katika maeneo mbalimbali yenye Wateja wengi wanaohitaji huduma hiyo.

Alitoa agizo hilo akiwa katika ziara ya kazi kwenye maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ulanga, Mkoani Morogoro.

Naibu Waziri alisisitizia kauli yake hiyo na kuwaagiza Meneja wa Kanda na Mkoa, kuandaa Mradi mdogo unaolenga kuwapelekea umeme Wananchi wa eneo hilo mapema iwezekanavyo, kabla hawajafikiwa na Mradi wa Ujazilizi.

“Nawaachia kazi hii, muandae Mradi wa kuwaletea Wananchi hawa umeme. Nimeona uwezo wa kulipa wanao na wamesubiri kwa muda mrefu sana. Wako tayari.” Alisema Mhe. Mgalu.

Kabla ya kutoa agizo hilo, Mhe. Mgalu  aliwauliza Wananchi ikiwa wako tayari kupelekewa huduma hiyo na TANESCO kwa gharama ya shilingi 177,000 au wasubiri Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA IIIA) uwafikie ambao utawagharimu shilingi 27,000 tu; na kwa umoja wao walitaka wapelekewe umeme wa TANESCO kwa madai kuwa wanao uwezo wa kulipia.

Aidha, alikiri kukerwa na utendaji kazi duni uliooneshwa na Mkandarasi MBH, aliyekuwa akitekeleza Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) katika Mikoa ya Pwani na Morogoro; ambapo alieleza kwamba ndiyo sababu Serikali haijampatia tena kazi.

Kufuatia suala hilo, aliwaagiza watendaji wa TANESCO, kuandaa taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo na kuiwasilisha ofisini kwake Dodoma, kabla ya Ijumaa ijayo, Julai 20 mwaka huu.

“Natambua kuwa Mkandarasi husika alikwishalipwa lakini zipo fedha kidogo zilizosalia kukamilisha malipo yake. Tutafute utaratibu utakaowezesha kuhamishia fedha hizo TANESCO ili zisaidie kutekeleza Mradi wa Ujazilizi badala ya kumlipa mtu ambaye ametutia hasara kwa utendaji duni,” alisisitiza.

Pia, alitoa onyo kwa Wakandarasi wanaotekeleza Miradi mbalimbali ya Umeme Vijijini, hususan REA III, kuwa Serikali haitamvumilia yeyote atakayeharibu kazi kwa namna yoyote.
Aidha, sambamba na onyo hilo, alisema kuwa, Serikali itamuwajibisha pia Msimamizi wa Serikali wa Mradi husika, ambaye atabainika kushindwa kumsimamia ipasavyo Mkandarasi na kusababisha kutotekelezwa kwa Mradi kikamilifu.

Maelekezo mengine aliyoyatoa Naibu Waziri katika ziara hiyo, ni kwa TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuhakikisha wanaunganisha umeme katika maeneo yote yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano haitaki kuona wananchi ambao wamepitiwa na miundombinu ya umeme, wakiishia kuangalia tu nyaya na nguzo pamoja na kuzilinda huku wao wenyewe wakiwa hawana umeme.
“Hili ni agizo kutoka kwa viongozi wetu wa juu, wakiongozwa na Mheshimiwa Rais John Magufuli, hivyo kilichobaki ni utekelezaji wake.”

Naibu Waziri amekuwa katika ziara ya kazi kwa takribani wiki tatu, katika Mikoa mbalimbali nchini, kukagua utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi. Vijiji vingine alivyotembelea wilayani Ulanga, ambako ndiko amehitimisha ziara yake, ni pamoja na Chikwera, Kata ya Mwaya pamoja na Kijiji cha Makanga, Kata ya Vigoi.

Baadhi ya watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Makanga, Kata ya Vigoi, Wilaya ya Ulanga, Ijumaa Julai 13, 2018 akiwa katika ziara ya kazi.

Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga, akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kutoka kulia), Kijiji cha Makanga, Kata ya Vigoi, wilayani Ulanga, Ijumaa Julai 13, 2018 kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme.

Sehemu ya umati wa wananchi wa Ulanga, mkoani Morogoro, wakimsiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipowatembelea Ijumaa, Julai 13 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi na kuwaeleza mikakati ya Serikali kuwapelekea umeme wa uhakika.


No comments:

Post a Comment