November 8, 2016

TAARIFA KWA UMMA



Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa iliyotolewa katika vyombo mbalimbali vya habari kuhusu ombi la kurekebisha bei za umeme kwa mwaka 2017.
 
Ombi la mabadiliko ya bei za umeme liliwasilishwa EWURA kulingana na Agizo la kubadilisha bei za umeme la mwaka 2016 lililoanza kutumika tarehe 1 April 2016. Ifahamike kuwa bei za umeme (Electricity Tariffs) zinazotumika zilitolewa zitumike mpaka tarehe 31/12/2016, hivyo itakapofika Januari 2017, inatakiwa bei mpya za umeme (New Electricity tariff) kutolewa kwa mujibu wa sheria. 

Hivyo TANESCO ilitakiwa kufanya tathmini ya gharama  za uzalishaji , usafirishaji na usambazaji umeme na kupeleka mapendekezo hayo kwenye Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA), ili kupitiwa na kufanyiwa taftishi(kupata maoni ya wadau) ikiwa ni pamoja na Baraza la Ushauri la Serikali . Hivyo basi ikiwa bei za umeme    zitapanda au kutopanda, hiyo itategemea na mapitio ya tathmini ya gharama za kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme tulizo wasilisha EWURA.

TANESCO haiwezi kuamua yenyewe kupandisha au kutopandisha bei za umeme. Kwa mujibu wa sheria, EWURA inapaswa ifanye mapitio ya bei za umeme kwa kila robo mwaka (Periodic Tariff Adjustment).

Tunapenda Umma ufahamu kuwa kupanda au kushuka kwa gharama za umeme ni suala la kisheria na ni jambo la kawaida kwani bei ya umeme imeshawahi kushuka katika vipindi tofauti kwa mfano Mwaka 2015 (robo ya kwanza ya mwaka) bei ilishuka kwa asilimia 2.5.  Vivyo hivyo Mwezi Aprili mwaka 2016 pia gharama za umeme zilishuka kwa asilimia 1.6


IMETOLEWA NA:  Mhandisi FELCHESMI MRAMBA
                                    Mkurugenzi Mtendaji
                                     Shirika La Umeme Tanzania (TANESCO)
                                     08 Novemba 2016

No comments:

Post a Comment