Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Ruvuma
ameweka jiwe la msingi la mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa
kilovolti 220 kutoka Makambako hadi Songea pamoja na ujenzi wa jengo la Ofisi
ya TANESCO Mkoani Ruvuma.
Mheshimiwa Majaliwa amesema lengo la ziara hiyo ni
kuwatayarisha Wananchi juu ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na
Serikali huku akieleza msimamo wa Serikali ni maslahi ya nchi kwanza.
Aliongeza, mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano
katika Sekta ya Nishati, ni kuona mtandao wa umeme unaenea pote nchini, na katika Vijiji ambavyo ni vigumu kufikika
kwa miundombinu ya umeme Vijiji hivyo vitatumia umeme wa jua (Solar System).
Ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi TANESCO kupitia kwa
Mwenyekiti wake Dkt. Alexander Kyaruzi, Menejimenti ya TANESCO pamoja na
Wafanyakazi kwa kuunga mkono katika utekelezaji wa Sera za Serikali.
“Nimpongeze Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
TANESCO Dkt. Alexander Kyaruzi kwa namna Bodi inavyosimamia, hongera sana wana
TANESCO kwa kuunga mkono jitihada za Serikali”. Alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha, alisema amefarijika sana kwa kuhakikishiwa ujenzi
wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Makambako hadi Songea kukamilika mwishoni
mwa mwezi Agosti na jingo la Ofisi mwezi Machi mwaka huu.
Aliongeza kufika kwa umeme wa gridi kutafungua fursa
za kibiashara kwa Wananchi wa maeneo hayo hivyo kutokuwepo malalamiko ya
ukosefu wa ajira kwa watu kujiari, “Ndugu zangu Umeme ni fedha, Kuwepo kwa
Umeme ni Ajira tosha, hivyo tuwekeze katika biashara ndogo ndogo za kutuingizia
kipato”.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati Dkt.
Medard Kalemani alisema katika kipindi cha Miaka miwili ya Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano kumekuwa
na mafanikio katika sekta ya nishati nchini ambapo katika njia za kusafirisha
umeme mkubwa zimejengwa mbili ambazo ni mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa
kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga na mmradi wa njia ya kusafirisha
umeme wa kilovolti 220 kutoka Makambako Mkoani Njombe hadi Songea Mkoani Ruvuma wenye urefu wa
kilometa 250.
Aliongeza kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme
ya Makambako hadi Songea kutaipunguzia TANESCO gharama kwa kuacha kutumia mitambo
ya kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta katika vituo vya Songea, Mbinga Namtumbo
na Madaba .
No comments:
Post a Comment