September 26, 2021

TANESCO MPYA IMEZALIWA LEO, TUNATAKA IENDESHWE KIBIASHARA- Waziri Makamba

 

Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amesema ni wakati sasa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO kuanza kujiendesha kibiashara, kwa ufanisi ili kuchangia uchumi wa Taifa.

Mhe. Makamba amesema hayo leo Septemba 26, 2021 wakati akizungumza na Mameneja wa TANESCO wa ngazi ya Kanda, Mikoa, Wilaya na Makao Makuu. 

Aidha Mhe. Makamba amewatambulisha Wajumbe wa Bodi ya TANESCO wakiogozwa na Mwenyeki, Bw. Omari Issa, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Maharage Chande, walioteuliwa Septemba 25, 2021 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Wajumbe wa Bodi ya TANESCO waliotambulishwa ni pamoja na Bw. Nehemia Mchechu, Bi. Zawadia Nanyaro, Bw. Lawrence Mafuru, Mhandisi Cosmas Masawe, Balozi Mwanaidi Maajar, Mhandisi Abdallah Hashim,  Bw. Abubakar Bakhresa na Bw. Christopher Gachuma.

Mhe. Makamba amesema Bodi iliyochaguliwa ina wajumbe kutoka nyanja mbalimbali na watasaidia Shirika kufikia malengo.

 "Tunataka baada ya miaka mitatu Shirika liingie katika orodha ya mashirika bora, yenye thamani na yanayoheshimika Afrika" alisema Mhe. January Makamba

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Bw. Omari Issa, amesema atahakikisha Bodi inafanya kazi na kutimiza malengo yake kwa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa malengo na uwajibikaji.

 Mkurugenzi Mtendaji, Bw. Maharage Chande, ameeleza vipaumbele ambavyo ni masilahi ya rasilimaliwatu, Wateja wa Shirika na utekelezaji wa mipango, hivyo ameomba ushirikiano kutoka kwa wafanyakazi wa TANESCO.

"Nimhakikishie Mhe. Waziri tutahakikisha tunarudisha heshima ya Shirika na ufanisi kupitia ushirikiano wenu, hakuna Shirika lolote linalotoa huduma ya umeme zaidi yetu sisi, yamkini tuwape wateja wetu huduma wanayostahili", " alisema Bw. Maharage Chande

Meneja Mwandamizi Rasilimaliwatu, Bw. Francis Sangunaa, aliwahakikishia viongozi ushirikiano kwa niaba ya wafanyakazi wa TANESCO.
 



 

September 4, 2021

MIRADI YA KIMKAKATI YA NISHATI ITAKAMILIKA KWA WAKATI

 

Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali amesema miradi yote ya kimkakati ya umeme inayotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO itakamilika kwa wakati.

Bw. Mahimbali ameyasema hayo leo Septemba 03, 2021 katika ziara ya Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, kukagua vituo vya kuzalisha umeme kwa gesi vya Kinyerezi.

Amesema ziara ilijikita zaidi kwenye mradi wa Julius Nyerere, ambapo Sekretarieti iliweza kufahamu hatua zote za kuzalisha umeme hadi kuusafilisha.

"Leo tumewaonesha Kinyerezi complex ambayo ina Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension pamoja na Kinyerezi ll" amesema Bw. Mahimbila.

Ametoa pongezi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa inayoifanya katika kuendeleza miradi ya umeme nchini.

Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri inahitimisha leo ziara ya siku tatu kukagua miradi ya umeme, ziara ilianzia kwenye kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Zuzu Jijini Dodoma, njia ya umeme itakayojengwa hadi Chalinze na mradi wa kufua umeme kwa maji wa Julius Nyerere.





 

September 3, 2021

Mkandarasi JNHPP ameshalipwa trilioni 2.7

 


 Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema Mkandarasi anaetekeleza mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) Mw 2115 ameshalipwa jumla ya shilingi trilioni 2.7 kulingana na mpango kazi kati ya shilingi trilioni 6.5 anazotakiwa kulipwa hadi kukamilika kwa mradi.

Dkt. Mwinuka ameyasema hayo leo Ijumaa Septemba 03, 2021 katika ziara ya Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri, Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais Ikulu na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kwa upande wake Karani wa Baraza la Mawaziri, Bw. Nsubili Joshua amesema ameongozana na Maafisa wa Sekritarieti ili kujionea kazi inavyoendelea JNHPP.

Amesema mradi wamekuwa wakiufahamu kwenye makaratasi hivyo wamefika kujionea hali halisi na kuona kinachoendelea.

Ameongeza kuwa wameona mambo makubwa ambayo hawayajatarajia na kutoa pongezi kwa viongozi wakuu Serikalini kwa kuutekeleza mradi huo.

Awali akieleza lengo la ziara hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya utumishi wa umma, Bw. Lauren Ndumbaru amesema wamefanya ziara katika mradi na watumishi wa umma wa ngazi zote ili watumishi waweze kuona na kuthamini kazi ambayo Serikali inafanya katika ujenzi wa miradi ya kimkakati.

"Naamini kabisa mradi wa Julius Nyerere ukikamilika utaleta maendeleo makubwa katika Nchi yetu, niombe watumishi wa umma wafanye kazi kwa bili na waendelee kuiunga mkono Serikali ili tuone matokeo mapema" amesema Bw. Ndumbalo

Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali amesema Wizara ya Nishati imefarijika kutokana na Ofisi zote mbili kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere.

"Tunamshukuru Rais Samia Hassan kwa kuendelea kuuangalia mradi huu kwa jicho la kipekee kabisa, tunapata pesa za kuendeleza mradi kwa wakati na usimamizi mzuri, tutaendelea kuusimamia na kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati" amesema Bw. Mahimbila.

 






August 18, 2021

Hatua nyingine kubwa JNHPP

 

Kazi ya usimikaji wa bomba (Draft tube) sehemu ya chini kabisa kwenye mashine nambari 9 imeanza Agosti 17, 2021, katika mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), bomba hizo zitatumika kutolea maji katika mitambo ya kufua umeme na kuyarudisha mto Rufiji kwa ajili ya matumizi mengine.

Hii ni hatua kubwa iliyofikiwa baada ya kukamilika kwa uundwaji wa bomba hizi zinazofungwa katika kitako cha msingi wa zege, kilichopo eneo la mita 42.7 juu ya usawa wa bahari.

Usimikaji wa bomba hizi ndio utawezesha kuanza kwa ufungaji wa sehemu za juu za mashine (turbine) na kisha jenereta za kufua umeme.

 




 

August 14, 2021

WAZIRI MKUU AKAGUA KITUO CHA TANESCO MSAMVU BAADA YA KUATHIRIKA NA MOTO

 

Waziri Mkuu wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, leo Agosti 14, 2021 amekagua kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro.

Mhe. Majaliwa amekagua athari zilizotokea baada ya kupata hitilafu iliyopelekea kuwaka moto kwa jumba la kudhibiti mifumo ya umeme wa msongo wa kilovolti 33 Agost 2, 2021.

Aidha, amewataka Wafanyakazi wa TANESCO kuendelea kufanya kazi kwa uaminifu na weledi kutokana na nishati ya umeme kuwa ndio injini ya ukuaji uchumi wa Nchi.

" Watumishi wa TANESCO mmebeba mioyo ya watu, muongeze umakini katika utendaji wenu wa kazi", amesema Mhe. Majaliwa.

Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa ameiagiza TANESCO Kufanya mapitio ya Wafanyakazi wanaosimamia vituo vya kupokea na kupoza umeme ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa weledi.

Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Msamvu mkoani Morogoro ni moja kati ya vituo 51 ambavyo vinapokea na kupoza umeme mkubwa wa gridi ya Taifa.

 





 

August 11, 2021

NAIBU KATIBU MKUU AKAGUA MRADI YA UMEME LUGURUNI

 


Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali, Agosti 07, 2021 alikagua utekelezaji wa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Luguruni Jijini Dar es Salaam.

Utekelezaji wa mradi wa Luguruni ulianza Aprili 01, 2020 na unatarajiwa kukamilika Septemba 30, 2021 ikiwa ni miezi 18 ya utekelezaji wa mradi.

Kukamilika kwa mradi wa Luguruni kutaboresha hali ya upatikanaji wa umeme katika Mikoa wa Pwani na Dar es salaam hasa kwa maeneo ya Kimara, Mbezi, Hospitali ya Taifa ya Mloganzila, msigani, kibamba, kibwegere, kisarawe, Maili moja na TAMCO (Industrial area) ambayo yamekuwa na changamoto ya kukosekana kwa umeme wa uhakika kutokana na njia za umeme zinanipeleka maeneo hayo kusafiri umbali mrefu.

Gharama za uzalishaji mradi wa Luguruni ni Shilingi Bilioni 15.2 ambazo zinagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 





MANUFAA YA KITUO CHA UMEME DEGE KWA KIGAMBONI NA MAENEO YA JIRANI


 Kituo cha kupokea na kupoza umeme  cha Dege ni mkombozi katika kukuza shughuli za kiuchumi na kijamii kwa Wilaya ya Kigamboni na maeneo jirani kutokana na kuimarisha upatikanaji wa umeme baada ya  kukamilika kwa utekelezaji wake Aprili 30, 2021.

Maeneo ya Viwandani, Pemba Mnazi, Mwasonga, Mwongozo, Kimbiji na maeneo jirani awali yalikuwa yanapata changamoto ya umeme kukatika au kuwa mdogo kutokana na njia ya umeme kusafiri umbali mrefu kutokea Mkoa wa kitanesco wa Ilala.

Akitembelea kituo hicho Agosti 07, 2021 Naibu Katibu Mkuu Nishati, Bw. Kheri Mahimbali ameridhishwa na usimamizi wa kituo cha Dege ambacho kilianza kujengwa Mei 02, 2019.

Aidha, mahitaji ya sasa ya Wilaya ya Kigamboni ni megawati 18 huku uwezo wa kituo cha Dege ni megawati 48 lakini malengo ya Serikali ni kukiongezea uwezo hadi hadi kufikia megawati 96.

 




 

August 10, 2021

TANESCO NA STAMICO WASAINI UTEKELEZAJI MRADI WA MAKAA YA MAWE KIWIRA

 


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) leo Agosti 10, 2021, limesaini hati ya makubaliano na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kuhusu utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 200 kwa kutumia makaa ya mawe ya Kiwira.

Akiongea wakati wa uwekaji saini Mkurugenzi Mtendaji TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka amesema utekelezaji wa mradi wa Kiwira utaenda sambamba na ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka ya urefu wa km 100 kutoka Kiwira hadi kituo cha kupokea umeme cha Mwakibete Mbeya.

Aliongeza kuwa, kwasababu mradi unagusa Taasisi mbili ni vyema kuwa na hati ya makubaliano ili kufahamu jukumu la kila Taasisi.

"STAMICO na TANESCO ni wadau wa mradi wa Kiwira, kwa maana kwamba STAMICO wao wanahusika na mgodi wa makaa ya mawe, TANESCO tutasimamia ujenzi wa mtambo wa kufua umeme", alisema Dkt. Mwinuka.

Amesema utekelezaji wa mradi wa Kiwira umeambatana na faida nyingi kwa Nchi ikiwemo uwepo umeme wa kutosha na kuweza kufanya biashara na Nchi jirani.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji STAMICO, Dkt. Venance Mwase amesema jukumu kubwa la STAMICO ni uchimbaji wa madini.

Serikali imekuwa ikisisitiza umuhimu wa Taasisi za Serikali kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo na hata kutoa huduma.

"Siku hii ya leo tumefikia makubaliano na TANESCO katika kuuendeleza mradi wa Kiwira kwa manufaa ya Taifa ", alisema Dkt. Mwase.








July 1, 2021

TANESCO YAENDELEA KUIMARISHA MFUMO WA LUKU

 Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka Juni 29, 2021 akizungumza na vyombo vya habari katika Ofisi za TANESCO Mikocheni Jijini Dar es Salaam amesema kuwa, kazi ya kuimarisha mfumo wa kuuza umeme wa malipo ya kabla (LUKU) bado inaendelea na maboresho ili kuimarisha zaidi uwezo wa mfumo huo kwa kuuongeza mfumo mbadala (backup).

Dkt. Mwinuka ameyasema hayo alipokutana na Waandishi wa habari kutolea ufafanuzi jinsi TANESCO inavyojipanga kuondokana na changamoto ya kukosekana kwa mfumo wa manunuzi ya umeme pamoja na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme nchini.

Aidha, Dkt. Mwinuka ameongeza kuwa, mfumo huo wa LUKU ulianza kufanya kazi Mei 19, 2021 mchana baada ya kutokea kwa hitlafu ya manunuzi ya umeme Mei 17 na 18, 2021 na hivi sasa kazi ya kujenga mfumo mbadala inaendelea.

"Hivi sasa tunaendelea na kazi ya kuhamisha taarifa kutoka kwenye mfumo wa msingi kupeleka kwenye mfumo mbadala baada ya kuukamilisha kuujenga" amesema Dkt. Mwinuka.

Ameongeza kuwa, katika kipindi hiki cha maboresho ya mfumo kutakuwa na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika manunuzi ya umeme kutokana na majaribio katika mfumo mbadala.

Amesema iwapo wananchi wanapata changamoto ya kununua umeme  kupitia mtandao mmoja, ni vyema kutumia mtandao mwingine pamoja na huduma za kibenki.

June 27, 2021

TANESCO YAWEZESHA MATIBABU MOI

 


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limechangia kiasi cha  Shilingi Milioni Ishirini kwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), ili kusaidia na kuwezesha matibabu ya watoto wenye vibiongo katika hospitali hiyo.

Akiongea katika Mbio fupi za kuchangia matibabu hayo (Moi marathoni) Juni 27,2021, katika viwanja vya chuo cha udaktari Muhimbili MUHAS, Meneja uhusiano wa TANESCO, Bi. Johary Kachwamba amesema kuwa  TANESCO imeona umuhimu wa kurudisha  kwa jamii sehemu ya kile inachokipata kupitia mauzo ya Umeme kwa kusaidia matibabu ya watoto hao.

"TANESCO imeamua kuangaza maisha ya jamii yetu kwa namna ya tofauti, tunafarijika kwamba matibabu haya yataokao uhai na kurejesha furaha kwa watoto wenye vibiongo" amesema Bi. Kachwamba

Sambamba na kuchangia kiasi hicho, wafanyakazi wa TANESCO pia wameshiriki katika kukimbia mbio hizo katika makundi ya km 5, km 10 na km 21, ambapo mshindi wa tatu mbio za km 5, kwa upande wa Wanaume ni Bw. Sebastian Kwayu, kutoka TANESCO.

Mgeni Rasmi aliepoke hundi kwa niaba ya MOI katika tukio hilo ni, Mhe. Tulia Akson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo alitoa shukrani kwa wote waliochangia ikiwa ni pamoja na TANESCO.

 






 

May 26, 2021

TANZANIA YAPATA DOLA MILIONI 140 UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME MARAGARASI

 

Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati na TANESCO, leo Mei 26,2021, imeingia makubaliano ya mkopo wa Dola milioni 140 kutoka Benki ya Maendeleo ya Africa (ADB) kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa kufua umeme wa megawati 49.5 kupitia maporomoko ya maji ya Mto Malagarasi uliopo Mkoani Kigoma.

Mradi wa Maragalasi utachochea ukuwaji wa shughuli za maendeleo ya kijamii pamoja na kiuchumi kwa wakazi wa Mikoa ya Kaskazini Mashariki mwa Tanzania.

Mradi huu, utahusisha pia uimarishaji gridi ya Taifa itakayorahisisha biashara ya mauziano ya Nishati ya umeme baina ya Tanzania na Nchi majirani.

Aidha gharama za mradi huo kwa ujumla ni takriban Dola milioni 144.14, ambapo Serikali ya Tanzania itachangia kiwango kinachobakia cha Dola milioni 4.14 kukamilisha fedha za Ujenzi wa Mradi huo muhimu kwa Mikoa ya ukanda wa Kaskazini Mashariki na Tanzania kwa ujumla.

May 1, 2021

KITUO CHA UMEME KIGAMBONI CHAKAMILIKA

 


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Aprili 30, 2021 majira ya saa 4:28 usiku limefanikiwa kuwasha kituo cha kupokea na kupoza  umeme cha Dege Kigamboni.

Ujenzi wa kituo cha kupokea umeme cha  Dege umefanywa na Wataalamu wa TANESCO, vifaa na mitambo vimeletwa na Mkandarasi Ms Telenergy d.o.o na njia ya umeme imejengwa na  Mkandarasi Kampuni ya JV Tontan Ltd Group Six.

Kuwashwa kwa kituo hicho cha Dege kumeenda sambamba na uwashaji wa umeme kwenye njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 132 kutoka kituo cha Mbagala hadi cha Dege.

Kituo cha Dege kinatarajiwa kuwa mkombozi wa changamoto za umeme kwa wakazi wa Kigamboni na maeneo jirani. 

Awali wananchi wa Kigamboni walipata umeme kupitia njia ndogo ya msongo wa kilovoti 33kV kutokea kituo cha Ilala na walikuwa wakikabiliwa na tatizo la umeme kukatika mara kwa mara pamoja na umeme kuwa mdogo. 

Baada ya kuwasha kituo hicho umeme wa uhakika utapatikana katika maeneo yote ya wilaya Kigamboni ikiwemo maeneo ya Kimbiji, Mwongozo, Mwasonga, Pemba mnazi, Kisarawe2, na maeneo ya Viwanda vikubwa Wilayani hapo.

Mradi wa  Dege ulianza kutekelezwa Mwezi Mei, 2019 kwa gharama ya shilingi 26.2 Bilioni.
 



 

April 27, 2021

WATAALAMU TANESCO KUENDELEA KUTEKELEZA MIRADI YA KIMKAKATI

 


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwa katika kikao kazi na Watendaji wa TANESCO leo Aprili 25, 2021 Jijini Dodoma, amesema mradi wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka Julius Nyerere hadi Chalinze kilometa 167 msongo wa kilovolti 400 utajengwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). 

Serikali imekuwa ikiwaamini na kuwatumia Wataalamu wa TANESCO katika kutekeleza na kusimamia miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwemo wa Julius Nyerere utakaofua megawati 2115.

Dkt. Kalemani ameongeza kuwa njia hiyo ya umeme inatarajiwa kukamilika mwezi mmoja kabla ya mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere kuakamilika. 

Katika hatua nyingine Dkt. Kalemani amesema kuwa, Serikali imeridhishwa na utendaji kazi wa Wafanyakazi wa TANESCO na Wizara ya Nishati imekuwa ikijivunia utendaji kazi wao. 

"Ndugu zangu mafanikio ya nchi hii yanategemea TANESCO, vigezo vilivyofanya tuingie kwenye uchumi wa kati umeme umechangia kwa kiasi kikubwa sana" amesema Dkt. Kalemani. 

Maeneo ambayo TANESCO imekuwa na mafanikio ni eneo la kuunganisha Wateja ambapo TANESCO iliweka malengo ya kuunganisha Wateja 300,000 na kabla ya mwezi Juni mwaka huu wamesha unganishwa Wateja 322,000 hivyo kuvuka lengo.

Eneo lingine ni ukusanyaji wa madeni sugu ya Serikali na Taasisi za umma deni lilikuwa bilioni 278 ambapo zimekusanywa bilioni 126.

Dkt. Kalemani amesema katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha wa 2020/21 Wizara imeainisha vipaumbele ambavyo ni utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya kufua umeme na kuyafikishia umeme wa gridi ya Taifa maeneo ambayo haijafika.