Ujenzi Kinyerezi 1
wakamilika kwa asilimia 50
Ujenzi wa mradi wa Kituo cha
Kufua umeme kwa kutumia gesi asilia Kinyerezi 1 ambao upo chini ya Mpango wa
taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) umekamilika kwa asilimia 50. Kituo hicho ambacho
kitakuwa na uwezo wa kufua megawati 150 baada
ya kukamilika kinategemea kutumia gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Mradi wa ujenzi wa bomba la gesi nao unakwenda kwa kasi.
Baada ya kukamilika kwa Mtambo
huu, kutakuwa na njia mbili za kusafirisha umeme ambapo njia moja ya msongo wa
kilovolti 132 itapeleka umeme kwenye Kituo cha Kupooza na kusambaza umeme cha
Gongo la mboto na viwandani na njia ya pili ya msongo wa kilovolti 220 itapeleka
umeme moja kwa moja kwenye gridi ya Taifa. Mradi huu unajengwa na kampuni ya
Jacobsen Elektro ya Norway.
Akizungumzia ujenzi huo Meneja wa
Kituo hicho, Mhandisi Simon Jilima alisema ujenzi huo umefikia katika hatua nzuri
na unategemewa kukamilika mwishoni mwa
mwaka huu ambapo mwezi wa tisa inategemewa kuanza majaribio ya kufua umeme. Aliongeza
kuwa mitambo hiyo imejengwa kisasa ambapo hata moshi unaotoka kwenye mitambo
hiyo ni kidogo sana kiasi kwamba hauna madhara kwa wananchi wanaoishi pembezoni
mwa mtambo na haina kelele.
Alisema, Mtambo huu umejengwa kwa
pesa ya serikali na umegharimu jumla ya dola za Marekani milioni 183 sawa na
shilingi bilioni 293 pesa ya kitanzania. Ujenzi wa Mradi huo pia umesaidia
kutoa ajira kwa watanzania wazawa ambapo asilimia 93 ya wafanyakazi ni
watanzania. Aidha Mhandisi Jilima alibainisha kuwa baada ya kukamilika kwa
mradi huo, wananchi wanaoishi pembezoni mwa mtambo huo wataweza kupata huduma
ya maji bure.
Mhandisi Jilima aliongeza kuwa, mtambo huu pia utakuwa na uwezo wa kufua
umeme kwa kutumia mafuta ambapo yanajengwa mantenki yenye uwezo wa kuchukua
lita milioni moja na nusu, akieleza sababu ya kutumia mafuta kuwa endapo kutakuwa
na matengenezo ya visima vya gesi kwa upande wa Shirika la Maendeleo ya Petroli
(TPDC) au matengenezo kwenye mashine za kusukuma gesi, mitambo hiyo itatumia mafuta
ili tusipoteze megawati 150 kwenye gridi ya taifa.
Eneo litakuwa na vituo vinne. Kinyerezi
1 itakayofua umeme megawati 150, Kinyerezi 2 kitakachofua umeme megawati 240,
Kinyerezi 3 kitakachofua umeme megawati 600 na Kinyerezi 4 kitakachofua umeme
megawati 330, mitambo yote itaendeshwa kwa gesi itakayomilkiwa na TPDC.
Mradi wa ujenzi wa mitambo ya
kufua umeme ya Kinyerezi 1-4 ni sehemu ya utekelezaji wa miradi iliyo chini ya
mpango wa taifa wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
No comments:
Post a Comment