November 3, 2014

MRADI WA UJENZI WA NJIA MPYA YA UMEME WA MSONGO WA KILOVOTI 400



MRADI WA UJENZI WA NJIA MPYA YA UMEME WA MSONGO WA KILOVOTI 400 UTAKAOUNGANISHA TANZANIA NA KENYA KUTOKA NAMANGA HADI SINGIDA KUPITIA ARUSHA NA BABATI

 

UWASILISHAJI WA TAARIFA YA TATHMINI YA ATHARI YA MAZINGIRA NA JAMII (ENVIRONMENTAL AND SOCIAL IMPACT ASSESSMENT STUDY), MPANGO WA KUHAMISHA MAKAZI (RESETTLEMENT ACTION PLAN) NA MPANGO WA USIMAMIZI WA RASILIMALI ZA UTAMADUNI (PHYSICAL CULTURAL RESOURCES MANAGEMENT PLAN) NA RIPOTI ZA ZIADA ZA WANYAMA PORI NA NDEGE.       


 

1. UTANGULIZI


Serikali kupitia TANESCO ina mpango wa kujenga njia mpya ya umeme mkubwa wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Namanga hadi Singida kupitia mikoa ya Arusha na Manyara na pia kuunganisha na gridi ya jirani zetu wa Kenya. Njia hii pia itaunganishwa na njia nyingine ya kilovoti 400 kutoka Dar es Salaam (Kinyerezi) hadi Arusha kupitia Chalinze, Segera na Tanga kwenye kituo hicho cha kupozea umeme. Nia na madhumuni ya mradi huu ni kuboresha upatikanaji na kuongeza nguvu ya umeme unaosafirishwa kutoka kwenye mitambo yetu ya ufuaji wa umeme kwenda kwenye maeneo ya wateja wa mikoa ya Kaskazini, Kaskazini Mashariki na Magharibi. Pia kuunganisha njia za umeme mkubwa na majirani zetu wa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kupitia Kenya na Zambia ambao utarahisisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika nchi zetu kwa kuuziana nishati hiyo na hivyo kukuza uchumi na kupunguza umaskini kwa wananchi wetu.

1.1 Kazi zitakazofanyika kwenye mradi huu ni :-

·   Kujenga njia ya umeme mkubwa wa kilovoti 400 ya takribani kilomita 415 kutoka Namanga hadi Singida kupitia mikoa ya Arusha na Manyara
·   Kusambaza umeme kwenye vijiji ambavyo njia hiyo itapita, na
·   Kujenga kituo kipya cha kupozea umeme cha kilovoti 400 cha Arusha eneo la Remugur na kuboresha kituo cha kupozea umeme cha Singida kufikia kiwango cha kilovoti 400
·   Kutekeleza mpango uliopitishwa wa kuboresha uharibifu wa kimazingira na jamii
·   Ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopitiwa na Mradi.

1.2 Matarajio ya mradi ni :-

·   Kuunganisha njia kubwa za umeme na majirani zetu wa Kenya na Zambia hatimae nchi zote za Afrika Mashariki na Kusini mwa jangwa la Sahara. Pia itarahisisha mpango wa kuuziana umeme na upatikanaji wa umeme wa uhakika na endelevu,  
·   Kuongeza nguvu na ufanisi wa usafirishaji wa umeme kutoka kwenye mitambo ya uzalishaji kwenda kwa wateja,
·   Kuboresha nguvu ya umeme katika laini za usafirishaji zilizopo na hivyo kuboresha nguvu ya umeme inayowafikia wateja,
·   Kupunguza upotevu wa umeme kwenye njia kuu za usafirishaji wa umeme,
·   Ongezeko la kuunganisha wateja,
·   Kuboresha huduma ya umeme kwa wateja wakubwa na wadogo kwa kupata umeme wenye ubora na kiwango hatimaye TANESCO kuwa na taswira nzuri na kupunguza malalamiko kutoka kwa wateja,
·   Kuendelea kuboresha na kupunguza umaskini wa maisha ya mtanzania kama inavyoelekezwa kwenye Mpango Mkakati wa Kupunguza na Kukuza Uchumi Tanzania (MKUKUTA).

1.3 Utayarishaji wa ripoti za utafiti :-
TANESCO ilifanya tafiti na kutayarisha ripoti mbalimbali kuona kama mradi huu unafaa kitaalam, kiuchumi na kifedha, kimazingira na kijamii.

TANESCO imekamilisha ripoti zilizotajwa hapo juu kama inavyoelekezwa kwenye miongozo ya Sheria na Kanuni za Tanzania, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA).


1.4 Uwasilishaji wa ripoti kwa umma  :-
TANESCO kupitia tangazo hili inapenda kuujulisha na kuwasilisha kwa umma taarifa zifuatazo za mradi:-

·               Tathmini ya Athari ya Mazingira na Jamii (Environmental and Social Impact Assessment Study) ya Mwezi wa Novemba 2013
·               Mpango wa Uhamishaji Makazi ya Mwezi  Februari 2013

·               Mpango wa Usimamizi wa Rasilimali za Utamaduni ya Mwezi Novemba 2013

·               Tathmini ya Athari ya Wanyamapori (hasa Tembo) na Ndege kwenye njia za wanyama na ndege maeneo Mradi utakapopita

·               Mpango wa watu wenye uhitaji maalum

·               Muhtasari wa Tathimini ya Athari ya Mazingira na Jamii

 

 Taarifa na ripoti za mradi zinapatikana katika sehemu zifuatazo:-

·         Maktaba ya TANESCO Makao Makuu, Ubungo
·         Maktaba Kuu ya Taifa – Mtaa wa Bibi Titi Mohamed - Dar es Salaam  
·         Tovuti ya TANESCO www.tanesco.co.tz nenda ”Investment” na kisha bonyeza  “Environmental reports”  
·         Ofisi za Wakuu wa Mikoa / Maafisa Tawala wa Mikoa ya Arusha, Manyara, na Singida 
·         Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida
·         Ofisi za Wakurugenzi wa Wilaya za Longido, Arusha, Monduli, Babati, Hanang na Singida

Pia nakala za Muhtasari wa  Tathmini ya Athari ya Mazingira na Jamii kwa lugha ya Kiswahili imewasilishwa kwenye ofisi zote za kata na serikali za vijiji ambapo njia ya umeme inategemea kupita.

1.5 Mawasiliano au Maulizo:-

Kwa ajili ya mawasiliano au maulizo ya ziada na kupata ufafanuzi juu ya mradi huu, wasiliana na Naibu Mkurugenzi Mtendaji – Uwekezaji, Msimamizi wa Mradi na Meneja Mwandamizi Utafiti, TANESCO Makao Makuu - Ubungo, S.L Posta 9024 Dar es Salaam; maulizo, maoni na ufafanuzi uwasilishwe kabla ya siku 21 baada ya tarehe ya tangazo hili kutoka kwenye magazeti.

TANESCO inauomba umma kusoma ripoti hizo na kuwasilisha maoni kwa ajili ya uboreshaji wa mradi kama yapo. Maoni yawasilishwe kwenye ofisi zifuatazo:-

1.   TANESCO Makao Makuu Dar es Salaam – Naibu Mkurugenzi Mtendaji – Uwekezaji, Meneja Mwandamizi Utafiti na Msimamizi wa Mradi.
2.   Ofisi za Mameneja wa TANESCO wa Mikoa ya Arusha, Manyara (Babati) na Singida.
3.   Ofisi za Mameneja wa TANESCO wa Wilaya za Longido, Monduli na Hanang.


Imetolewa na:      Ofisi ya Uhusiano,
TANESCO MAKAO MAKUU - DAR ES SALAAM

No comments:

Post a Comment