April 10, 2014

TAARIFA

TAARIFA KWA UUMA KUHUSU
UTAPELI UNOFANYWA NA BAADHI YA WATU KUPATA HUDUMA ZA TANESCO
Kumeibuka utapeli unaofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu kuwarubuni wananchi wanaotaka kufungiwa umeme katika makazi yao kwa kuwadanganya kwamba wanaweza kuwasaidia kufungiwa umeme haraka iwezekanavyo bila kuchelewa, huku wakiomba fedha kutoka kwa wananachi hao.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linapenda kuwataarifu wananchi wanaomba huduma ya kufungiwa umeme na wateja wake kote nchini kuwa wasikubali hata kidogo kurubuniwa na mtu yeyote anayejifanya eti akipewa fedha ndipo mteja atafungiwa umeme haraka. Shirika linatumia utaratibu wa “FIFO First In First Out” yaani mteja anayeomba huduma ya umeme kwanza ndiye anayefungiwa kwanza. Utaratibu huu uko wazi kwa kila mkoa kubandika majina ya wateja waliomba huduma ya umeme na tarehe ya kufungiwa kwenye mbao za matangazo.
Aidha, matapeli hao huwadanganya wananchi kuwa punguzo la gharama za kuunganisha umeme liliotolewa na Serikali Januari mwaka jana nila muda mfupi. Tupenda kusisitiza kwamba punguzo hili la gharama ya uunganishaji wateja kote nchini halina kikomo na ni endelevu isipokuwa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara tu. Hivyo mtu yeyote asikubali kudaganywa, malipo yote yafanyike katika ofisi za TANESCO na si vinginevyo. Na baada ya mteja kulipia, ahakikishe anapewa stakabadhi iliyoandikwa kwa kompyuta na si kwa mkono.
Uamuzi wa kupunguza gharama za kuwaunganishia wananchi umeme ulifikiwa na serikali katika Bunge la bajeti la mwaka 2012 ili watu wengi mijini na vijijini waweze kujipatia nishati hii kwa gharama nafuu.
Hivyo, Serikali kupitia TANESCO imepunguza gharama za kuunganisha umeme wa njia moja (single phase) kwa wateja wadogo mijini  kwa wastani wa asilimia 30 na punguzo la wastani wa asilimia 70 kwa wateja wa vijijini kuanzia mwezi Januari, mwaka jana. Kwa kufanya hivyo, wateja wengi wamemudu gharama na hatimaye kuongeza kasi ya kuunganisha umeme. Hadi kufikia Desemba 2013 Shirika liliweza kuunganisha wateja 143,469 tofauti na mwaka juzi ambapo liliunganisha wateja 88,114 ikiwa ni ongezeko la asilimia 62. 
Gharama za kuomba kuunganishiwa umeme ni kama ifuatavyo:
Kwa wateja wanaoomba kuunganishiwa umeme wa njia moja (single phase) kwenye umbali usiozidi mita 30 na bila kuhitaji nguzo, katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 177,000 na wa mijini watalipa Shilingi 320,960 badala ya Shilingi 455,108 zilizokuwa zinalipwa awali. Punguzo hili ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa wateja waishio  mijini. 
Kwa wateja wanaoomba kuunganishiwa umeme wa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja, katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 337,740 na wa mijini watalipa Shilingi 515,618 badala ya Shilingi 1,351,884 zilizokuwa zinalipwa awali. Punguzo hili ni sawa na asilimia 75.02  kwa wateja waishio vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio  mijini.
Aidha, kwa wateja wanaoomba kuunganishiwa umeme wa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini watalipa Shilingi 454,654 na wa mijini watalipa Shilingi 696,670 badala ya Shilingi 2,001,422 zilizokuwa zinalipwa awali. Punguzo hili ni sawa na asilimia 77.28  kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio  mijini.
Katika mikoa mipya ya Simiyu na Geita ambapo kuna miradi mingi ya umeme vijijini, kuna matapeli wanapita kuwachangisha fedha wananchi na kuwaahidi kuwapelekea umeme. Tunawaomba wananchi wawe makini na watu hao na kutoa taarifa kwenye serikali za vijiji au vyombo vya usalama kwani TANESCO haichangishi watu mitaani ili kuwaletea huduma ya umeme.
Aidha, kuna baadhi ya watoa huduma, wanaouza umeme kwenye vituo mbalimbali nchini ambao wanawatoza wateja pesa zaidi ya ile inayooneka kwenye risiti ya kununulia umeme. Tunawakumbusha wananchi na wateja wote wanaonunua umeme wa mita za LUKU kupitia kwa mawakala wetu, kwamba hakuna mteja anayepaswa kukatwa pesa zaidi kwa ajili ya kupata huduma za umeme wa mita za LUKU. Makato yote ya umeme yanatakiwa kuonekana kwenye skabadhi ya mteja anaponunua umeme.
Uongozi wa Shirika umefanya mawasiliano na vyombo vya usalama kwa ajili ya uchunguzi na kuwashughulikia matapeli hao kwa vitendo hivyo ambavyo vinaendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Tunawaomba wateja na wananchi wote kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa TANESCO pale wanapowabaini watu hao wanaotumia jina la Shirika vibaya na kwa maslahi yao binafsi kwa kupiga simu na +255 222 451185 au barua pepe: communications.manager@tanesco.co.tz au kwa kutumia twitter www.twitter.com/tanescoyetu au watoe taarifa Ofisi yoyote ya TANESCO iliyo karibu au Kituo chochote cha Polisi.
Imetolewa na:
Ofisi ya Uhusiano,
TANESCO Makao Makuu.

No comments:

Post a Comment