October 3, 2014

ZAMBIA, TANZANIA , KENYA KUIMARISHA MTANDAO WA UMEMECOMESA- yaeleza ni mradi wa kimaendeleo Afrika
     Mawaziri   wa Nishati kutoka nchi za Zambia, Tanzania na Kenya wakisaini Mkataba wa Makubaliano kuonesha dhamira ya Serikali ya nchi hizo kujenga miundombinu ya pamoja ya kusafirisha umeme na kufanya biashara ya kuuziana umeme wa ziada baina ya nchi hizo. Mkataba huo ulisainiwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nishati na Madini Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo (katikati), Waziri wa Wizara ya   Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji  wa Zambia , Christopher Yaluma (kushoto)  na  Waziri wa Nishati na Petroli Kenya , Davis Chirchir (kulia) . Wanaoshuhudia kutoka kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Migodi , Nishati na Maendeleo ya Maji Zambia, Charity Mwansa, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini , Tanzania , Eliakim Maswi na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Petroli Kenya,  Mhandisi Joseph Njoroge.

      Mawaziri wa Nishati kutoka nchi za Zambia, Tanzania na Kenya , kutoka kushoto Waziri wa  Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji  wa Zambia , Christopher Yaluma, Waziri wa Nishati na Madini Tanzania , Profesa Sospeter Muhongo Tanzania na Waziri wa Nishati na Petroli Kenya, Davis Chirchir) wakibadilishana Mkataba wa Makubaliano kuonesha dhamira ya Serikali ya nchi hizo kujenga miundombinu ya pamoja ya kusafirisha umeme na kufanya biashara ya kuuziana umeme wa ziada baina ya nchi hizo mara baada ya kusaini.

       Mawaziri wa Nishati kutoka nchi za Zambia, Tanzania na Kenya , kutoka kushoto  ni Waziri wa  Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji  wa Zambia , Christopher Yaluma Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo  Tanzania na Waziri wa Nishati na Petroli Kenya, Davis Chirchir wakionesha Mkataba wa Makubaliano mara baada ya kusaini.

     Sehemu ya Washiriki walihudhuria hafla ya kusaini Mkataba wa Makubaliano kuonesha dhamira ya Serikali ya nchi za Zambia, Tanzania na Kenya kujenga miundombinu ya pamoja ya kusafirisha umeme na kufanya biashara ya kuuziana umeme wa ziada baina ya nchi hizo. Mbali na Wataalamu kutoka katika nchi hizo, hafla hiyo imehudhuriwa uwakilishi wa COMESA,  Mashirika ya Umeme kutoka nchi hizo na  baadhi ya washirika wa Maendeleo wakiwemo Benki ya Dunia, Umoja wa Ulaya, Ubalozi wa Norway, Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Ubalozi wa Ufaransa.

Asteria Muhozya, Dar es Salaam                            
Nchi za Zambia, Tanzania na Kenya zimesaini  Mkataba wa Makubaliano  kuonesha dhamira ya Serikali ya nchi hizo kujenga kwa pamoja  miundombinu ya ya kusafirisha umeme na kufanya biashara ya kuuziana umeme wa ziada baina ya nchi  hizo (ZTK) .
 Makubaliano hayo yalisainiwa  jijini   Dar es Salaam tarehe  30 Septemba, 2014,  na Mawaziri wa Nishati kutoka nchi hizo ambao ni Waziri wa Nishati na Madini  wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji wa Zambia, Christopher Yaluma na Waziri wa  Nishati na Petroli wa Kenya Davis Chirchir.
Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Nishati na Madini, Tanzania Profesa Sospeter Muhongo alieleza kuwa, utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umeme unalenga kuondoa tatizo la upungufu wa nishati ya umeme kwa nchi hizo na barani Afrika. Profesa Muhongo  alisema  ambalo litachangia katika kukuza uchumi wa mataifa hayo, ikizingatiwa kuwa, nchi nyingi za Afrika bado zina uhaba wa nishati ya umeme,   ambayo ni kichocheo kikuu cha maendeleo, hivyo, utekelezaji wake  unatarajiwa kuziunganisha nchi za  Kusini , Mashariki na Kaskazini mwa Afrika na nishati hiyo.
Prof.Muhongo aliongeza kuwa, ili nchi hizo ziweze kufanya biashara ya kuuziana umeme itajengwa miundombinu ya pamoja ya kusafirisha umeme katika nchi zote na kuongeza kuwa, mkutano huo umekubaliana kwamba, kila nchi itabeba jukumu la kujenga miundombinu ya mradi huo lengo likiwa kuhamasisha ushindani na kuwezesha upatikanaji rahisi wa umeme katika nchi hizo.
“Ili umeme uweze kuuzwa, lazima kila nchi ijenge miundombinu ya kusafirisha umeme huo. Tukumbuke kwamba, umeme utakaouzwa ni wa ziada. Kwa hivyo, Tanzania itajenga miundombinu yake vivyo hivyo kwa Zambia na Kenya”, alisisitiza Muhongo.
Akizungumzia jitihada zilizofanywa Tanzania  katika utekelezaji wa mradi huo, alieleza kuwa, bei ya umeme nchini bado ni ghali kutokana na matumizi ya mafuta yanayotumika kuzalisha umeme na kuongeza kwamba, Tanzania tayari imeanza utekelezaji wa mradi huo kwa ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa- Dodoma- Singida- na Shinyanga (backbone) ambao ni sehemu ya mradi huo.
Vilevile, Waziri Muhongo aliongeza kuwa, uwezeshaji wa ujenzi wa mtandao wa umeme wa msongo wa kilovati 400 wa mradi wa Singida- Arusha hadi Namanga  (Tanzania) na Namanga Isinya Kenya unaendelea , wakati uchambuzi yakinifu wa ujenzi wa mtandao wa umeme  wa njia ya Mbeya - Kasama Tanzania tayari umekamilishwa na kinachofanyika hivi sasa ni kutafuta fedha za kukamilisha ujezi  wa mradi huo.
“Mradi kwa nchi hizi tayari umeanza kutekelezwa. Makubaliano ya awali hayakuruhusu ushindani. Tumeboresha namna tutavyotekeleza mradi huo. Tutatekeleza kwa pamoja lakini kila nchi itautekeleza mradi huu kipekee,” alibainisha Waziri Muhongo.
Aidha, Muhongo alisisitiza kuwa, hakuna haja ya nchi hizo kuendelea kuwa na upungufu wa nishati ya umeme ikizingatiwa kuwa, nchi hizo zinayo rasilimali ya kutosha yakiwemo makaa ya mawe, nishati jadidifu ikiwemo jotoardhi na gesi asilia.
Naye,  Waziri wa Migodi, Nishati na Maendeleo ya Maji  wa Zambia , Christopher Yaluma alieleza kuwa, utekelezaji wa mradi huo sio tu utaziwezesha nchi hizo kufanya biashara bali pia utafungua fursa za uwekezaji na kusaidia katika kuondoa umaskini miongoni mwa nchi wanachama kutokana kuzitumia fursa mbalimbali zinazotokana na nishati ya umeme.
Waziri Yaluma aliongeza kuwa, pamoja na kwamba mashauriano ya utekelezaji wa mradi huo yalichukua miaka mingi kuanza kutekelezwa, hivi sasa nchi hizo zimeazimia kuhakikisha kwamba mradi huo unatekelezwa.
Kwa upande wake Waziri wa Nishati na Petroli Kenya, Davis Chirchir aliwataka washirika wa maendeleo kusaidia katika kuwezesha utekelezaji wa mradi huo wa kujenga miundombinu ya pamoja ya kusafirisha umeme baina ya nchi hizo kutokana na manufaa yake kwa bara la Afrika na kuongeza kuwa, kutokana na uwepo wa rasilimali asilia za kutosha katika nchi hizo hakuna sababu ya kuwepo tatizo la nishati katika nchi hizo na barani Afrika.
Naye, Katibu Mkuu Msaidizi  wa Jumuiya ya Soko  la pamoja la nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) anayeshughulikia miradi Dkt. Kipyego Cheluget alizipongeza nchi hizo kwa kuuendeleza utekelezaji wa mradi huo ambao umechukua kipindi kirefu na kuueleza kuwa, ni miongoni mwa miradi 16 ya kipaumbele na kimaendeleo kwa Afrika.
Aidha, kwa upande wao Washirika wa maendeleo waliohudhuria hafla hiyo, walionesha kufurahishwa kwao na dhamira ya nchi hizo na kuahidi kushirikana na nchi hizo kuhakikisha mradi huo unatekelezwa. Miongoni mwa washirika wa maendeleo waliohudhuria ni pamoja na uwakilishi wa Umoja wa Ulaya, Benki ya Dunia, Ubalozi wa Norway,  Shirika la Maendeleo la Japani (JICA), African Development Bank(AfDB) na Ubalozi wa Ufaransa.
Mkataba rasmi wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kusafirisha na kuuziana umeme, unatarajiwa kusainiwa ifikapo tarehe 3 Novemba, 2014 nchini Zambia. Njia za ujenzi wa miundombinu hiyo ya kusafirisha umeme zinajengwa kutoka nchini Kenya, kupitia  Tanzania hadi Zambia, ambapo Mawaziri wa  nchi husika   walikubalina kukamilisha utekelezaji wake ifikapo mwishoni mwa  mwaka 2016.


No comments:

Post a Comment