July 10, 2014

Kukanusha habari iliyochapishwa gazeti la nipasheKatika toleo lake la Jumanne Julai 8, 2014 Gazeti la Nipashe katika ukurasa wa tano (5) lilichapisha taarifa yenye kichwa cha habari “Bodi TANESCO yapinga Baraza la Mawaziri”.  Kwa mujibu wa gazeti hilo ni kwamba taarifa hiyo imetolewa na anayesemekana kuwa ni mjumbe wa Bodi ambaye hakutaka  jina lake litajwe.

Nikiwa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kwa niaba ya wakurugenzi wa bodi ya TANESCO ninakanusha vikali kuwa taarifa hiyo si ya kweli, ni ya kupotosha umma na haina maslahi yoyote kwa maendeleo ya taifa letu. Aidha napenda kukanusha vikali kuwa taarifa hiyo haikutolewa na mjumbe yoyote wa Bodi ya TANESCO.

Kwa mukhtadha huo napenda umma wa watanzania ufahamu kuwa Bodi ya wakurugenzi na manejimenti ya TANESCO walishirikishwa kikamilifu katika hatua zote kuhusu nia ya serikali ya kuligawa shirika ili kuongeza ufanisi zaidi. Bodi na manejimenti ilifanya warsha ya siku tatu  Bagamoyo kwa ajili ya kujadili na hatimaye kufikia muafaka na kuandaa mapendekezo kuhusu jinsi ya kuligawa shirika. Mapendekezo hayo yaliwasilishwa rasmi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini.

Aidha mapendekezo yaliyopelekwa kwenye Baraza la Mawaziri ni maamuzi ya bodi ya TANESCO ambapo kabla ya  kufikishwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri, bodi ya TANESCO pamoja na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini ilikaa kupitia mapendekezo hayo kifungu kwa kifungu na kukubaliana juu ya mpango wa kuligawa shirika. Katika hali hiyo haiwezekani  kuwepo kwa mjumbe yoyote anayeweza kupinga mpango huo.

Kwa utaratibu ulivyo, maamuzi ya Baraza la Mawaziri ni agizo la serikali kwa taasisi zilizo chini yake. Kwa sababu hiyo hakuna ukweli wowote kuwa Bodi ya TANESCO inapinga maamuzi ya Baraza la Mawaziri.

Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, nakanusha kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na wala hazijatoka kwa mjumbe yeyote wa Bodi ya TANESCO. Napenda kuwahakikishia watanzania kuwa Bodi yangu inaafiki na itaendelea kutoa ushirikiano kwa serikali na taasisi zingine kuhakikisha kuwa maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusu mpango huo wa kuligawa shirika unatekelezwa kikamilifu na kwa wakati.


Imetolewa:
Gen. Robert Mboma (Rt)
Mwenyekiti wa Bodi
Kwa niaba ya Wakurugenzi wa Bodi ya TANESCO


No comments:

Post a Comment