October 25, 2013

Tusiisahau mitambo ya hydro-Wabunge


  • Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wameitaka Serikali na TANESCO kutoisahau na kuitelekeza mitambo inayotumia nguvu ya maji kutokana na mitambo inayotumia nguvu ya gesi kuanza kutumika.
    Wabunge hao waliyasema hayo wiki hii, walipofanya ziara katika mitambo inayotumia nguvu ya maji kuzalisha umeme ya New Pangani, Kidatu, Mtera na Kihansi ili kujionea hali ya mitambo hiyo na jinsi inavyochangia umeme katika gridi ya taifa.
    Mbunge wa Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela alisema kwa hakika wao kama wabunge hawakujua kama Serikali kupitia TANESCO imewekeza rasilimali kubwa na zenye thamani kwenye nchi kama ilivyo kwenye mitambo inayotumia nguvu ya maji kuzalisha umeme.
    “Mimi nasema nitapamba na yeyote atakayesema kwamba Serikali haikuwekeza, oneni jinsi utaalamu mkubwa ulivyotumika hapa na rasilimali nyingi zimewekezwa hapa kwenye mitambo hii”.
    “Tunaiomba Serikali kuangalia tulikotoka na ihakikishe mitambo hii haipuuzwi na kusahaulika eti kwa sababu sasa tumeanza kutumia mitambo ya gesi,  tusigeuke kuwa na tabia za wanaume wengi kwamba akioa mke mdogo basi humsahau na kumtelekeza mke mkubwa, sasa na sisi tusihau mitambo ya hydro”, alisema Mhe. Kilango kwa msisitizo.
    Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye ndiyo aliyekuwa kiongozi na Mwenyekiti wa msafara huo Mhe. Jerome Bwanausi alisema Wabunge wamejifunza mambo makubwa ambayo wasingeyajua kuhusiana na umeme kama wasingefanya ziara hiyo kwenye mitambo hiyo.
    Mhe. Bwanausi alisema kazi ya uzalishaji umeme, kuusafirisha hadi kumfikia Mwananchi ni kubwa tofauti na watu wengi wanavyodhani kwa hiyo ni muhimu kwa TANESCO kutoa elimu kwa wananchi kwa kuonyesha hatua zote ambazo umeme unapitia hadi kumfikia Mtanzania wa kawaida.
    “Ni muhimu sana kwa sisi wabunge na hata viongozi wa Serikali kutembelea mara kwa mara mitambo hii na kujiona hali halisi na maendeleo yake kwa kuwa hizi ni rasilimali kubwa za taifa letu”, alisisitiza Mhe. Bwanausi.
    Naye Mhe. Devotha Likokola alisema kutokana na uwekezaji mkubwa katika sekta ya umeme nchini ni muhimu kwa TANESCO kushirikiana na Wabunge hususan wa Kamati ya Nishati na Madini katoa elimu ya matumizi bora ya umeme kwani umeme ni gharama na uwekezaji wake unatumia rasilimali nyingi.
    “Nasema TANESCO acheni kukaa kimya tushirikisheni sisi wabunge ili tukawaeleze wabunge mambo mazuri yanayofanywa na TANESCO na pia juu ya matumizi bora ya umeme, sisi ndiyo wawakilishi wa wananchi, na mimi ndiyo nitakuwa wa kwanza kuwa balozi wa kutoa elimu hiyo najitolea,” alisisitiza Mhe. Likokola.
    Mhe. Juma Njwayo aliitaka TANESCO kushiriki katika kuisaidia jamii (Corporate Social responsibility) katika maeneo ambayo ya mitamboni ili wananchi waione hiyo mitambo ni mali yao kwa kuijali na kuilinda.
    Aidha, Mhe. Njwayo alisema kwamba mbali na jamii hata wafanyakazi ambao wanafanyakazi kwenye mitambo hiyo lazima wapewe vivutio vya kuwafanya wafanye kazi kwa moyo na wasijione kama wametengwa ama kupelekwa kwenye mitambo hiyo ni adhabu.
    Mhe. Dkt. Dalali Kafumu alisisitiza kwa wafanyakazi wa mitambo hiyo kupelekwa kusoma mara kwa mara kwa kuwa teknolojia ya mitambo hubadilika nayo kila wakati.
    Mhe. Murtaza Mangungu alisisiza kwa Serikali kuhakikisha mitambo hiyo inafanyiwa matengenezo haraka pale inapopata hitilafu badala ya kuicha na hatimaye taifa kupoteza mapato ambayo yangepatikana kwa uzalishaji umeme.
    “Ninasikitika sana kusikia kwamba mtambo mmoja wa Hale uliharibika tangu mwaka 2004 hadi leo umeachwa, tunataka Serikali itueleze kwa nini imefanya hivyo na lini mtambo huo wataurekebisha, ituambie ‘revenue loss’ kutokana na kuharibika kwa mtambo huo”, alihoji Mhe. Mangungu.


     Waheshimiwa Wabunge wakiwa katika ukumbi wa mkutano kwenye kituo cha Hale wakipata maelezo juu ya hali ya mitambo na namna inavyofanya kazi kuchangia umeme kwenye gridi ya taifa

     kutoka kushoto aliyevaa koti ni Meneja wa Mtamno wa New Pangani Mhandisi John Skauki akitoa maelezo kwa Wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini katika eneo la Bwawa la New Pangani Falls.
     kutoka kushoto aliyevaa koti ni Meneja wa Mtamno wa New Pangani Mhandisi John Skauki akitoa maelezo kwa Wabunge wa Kamati ya Nishati na Madini katika eneo la Bwawa la New Pangani Falls.
     katikati aliyenyoosha mkono ni Meneja anayesimamia mitambo ya umeme inayotumia nguvu ya maji Mhandisi Costa Rubagumya akitoa maelezo kwa wabunge waliofika kwenye Bwawa la New Pangani falls kuangalia hali ya maji kwenye Bwawa hilo.




     aliyenyoosha mkono ni Mhandisi wa New Pangani Bw. Makunga akiotoa maelezo ya jinsi mitambo ya maji inavyofanya kazi
     Katikati mwenye miwani ni mbunge wa Same Mashariki, Mhe. Anne Kilango Malacela na wenzake wakimsikiliza Mhandishi wa mitambo wa New pangani Falls akiwapa maelezo namna maji yanavyogonga turbine na umeme kuzalishwa


     

No comments:

Post a Comment